Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 01:15

Rais Paul Kagame wa Rwanda amefanya mabadiliko muhimu katika uwongozi wa jeshi


Rais Paul Kagame wa Rwanda
Rais Paul Kagame wa Rwanda

Rais wa Rwanda Paul Kagame amefanya mabadiliko muhimu kwenye idara zaa usalama nchini humo ambapo amemsimamisha kazi waziri wa ulinzi Meja Jenerali Albert Murasira na mkuu wa majeshi Jenerali Jean Bosco Kazura.

Nafasi ya waziri wa ulinzi imechukuliwa na Meja Jenerali Juvenali Marizamunda ambaye alikuwa ni afisa mkuu wa magereza. Rais Paul Kagame pia amemteua Luteni Jenerali Mubarakh Muganga kuwa mkuu wa majeshi akichukua nafasi ya Jenerali Jean Bosco Kazura ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo kuanzia mwezi Novemba mwaka 2019.

Katika maamuzi yake Rais Kagame amefanya pia mabadiliko kwenye idara ya upelelezi jeshini ambapo Meja Jenerali Vincent Nyakarundi ambaye alikuwa mkuu wa idara hiyo ameondolewa na kuteuliwa kuwa mkuu wa jeshi la nchi kavu.

Nafasi ya Meja Jenerali Vincent Nyakarundi imechukuliwa na mkuu wa zamani wa idara ya uhamiaji Kanali Francis Regis Gatarayiha ambaye hata hivyo anaikaimu nafasi hiyo.

MABADILIKO YAMEFIKA MSUMBIJI

Mabadiliko haya pia yameathiri muundo wa jeshi la Rwanda linalopigana kwenye jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Polisi wa Rwanda wapiga doria mjini Palma, jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji
Polisi wa Rwanda wapiga doria mjini Palma, jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji

Kagame amemteua Meja Jenerali Alex Kagame kuwa kamanda mkuu wa kikosi cha jeshi la Rwanda nchini Msumbiji akichukua nafasi ya Meja Jenerali Eugeni Nkubito ambaye anakwenda kuwa kamanda wa division ya 3 katika jimbo la magharibi mwa Rwanda linalopakana na Jamhuri ya Kidemokrais ya Kongo.

Kanali Theodomir Bahizi ameteuliwa kuwa kamanda mratibu wa shughuli za mapambano nchini Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado.

USALAMA WA KIKANDA

Jeshi la Rwanda limefanikiwa kuzima uasi wa makundi ya kighaidi nchini Msumbiji na sasa mabadiliko haya yanafanyika huku hali ya sintofahamu baina ya Rwanda na jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiendelea kuharibika kabisa kiasi cha kuzua hofu ya kutokea makabiliano baina ya nchi hizi jirani.

Wadadisi wanahisi kumtoa kamanda wa kikosi cha Rwanda nchini Msumbiji na kumpeleka kuwa kamanda wa majeshi jimbo la magharibi kunatoa ujumbe Fulani katika mzozo huo kati ya DRC na Rwanda.

Gari la kijeshi la Rwanda likiwa na wanajeshi wamekaa juu linapiga doria mjini Kigali Rwanda
Gari la kijeshi la Rwanda likiwa na wanajeshi wamekaa juu linapiga doria mjini Kigali Rwanda

Hadi sasa DRC inaishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23 huku Rwanda ikikanusha madai hayo na kwa upande mwingine inailaumu DRC kuwaunga mkono wanamgambo wa kihutu wa FDLR ambao Rwanda inawavisha jukumu la mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi mwaka 1994.

Kagame pia anafanya mabadiliko huku kukiendelea na tishio la usalama mdogo kwenye mpaka wake na DRC na uvumi kwamba huenda kukazuka mapigano mapya mashariki mwa DRC hali inayotoa tishio kwa usalama wa Rwanda

Hata hivyo hadi sasa hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu mabadiliko haya. Lakini hii imekuwa ni mara ya kwanza ambapo waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi kwa pamoja wakisimamishwa kazi.

Lakini pia wadadisi wanahisi pia Rais Paul Kagame kumteua Luteni Jenerali Mbarakh Muganga mmoja wa wanajeshi wazoefu na wenye kuheshimika nchini Rwanda kutokana na tajiliba yake katika vita huenda kuna sababu ambayo hadi sasa bado kujulikana.

Luteni Jenerali Mubarakh Muganga mwenye umri wa miaka 56 alipigana vita bega kwa bega na Rais wa Kagame wakati vya vita na mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi kuanzi mwaka 1990 hadi mwaka 1994 yaliposimamishwa.

Forum

XS
SM
MD
LG