Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:57

Zelenskyy atoa wito kwa washirika wa Magharibi; 'harakisheni ufikishaji silaha'


Wanajeshi wa Marekani wahudhuria hotuba ya ufunguzi ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy aliyotoa kwa njia ya video huko Ramstein, Ujerumani, Jan. 20, 2023.
Wanajeshi wa Marekani wahudhuria hotuba ya ufunguzi ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy aliyotoa kwa njia ya video huko Ramstein, Ujerumani, Jan. 20, 2023.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alikuwa na ujumbe rahisi kwa washirika wake wa Magharibi katika kongamano la wahisani Ijumaa nchini Ujerumani: “harakisheni ufikishaji wa silaha.

Akizungumza kwa njia ya video katika mkutano uliofanyika katika kambi ya Jeshi la Anga la Marekani, ambako washirika wa Ukraine walikusanyika kujadili njia bora ya kuisaidia Ukraine wakati ikikabiliana na uvamizi wa Russia uliodumu kwa karibu mwaka mzima, Zelenskyy alisema washirika hao wanahitaji “ kuacha kujadili kuhusu idadi mbalimbali ya vifaru, lakini kuanza kupeleka vitu muhimu ambavyo vitatokomeza udhalimu.”

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin aliyaambia mataifa fadhili, “Tunatakiwa kuzama kwa kina zaidi. Huu ni wakati muhimu kwa Ukraine.” Alisema, “Watu wa Ukraine wanatuangalia, Kremlin inatuangalia, na historia inatuangalia sisi.”

Mkutano huo ulijumuisha wawakilishi kutoka nchi 50, ikiwemo wanachama wote wa NATO.

Kabla ya mkutano wa Ijumaa, Marekani na Ujerumani zilionekana kama haziko tayari kupeleka vifaru aina ya Leopard 2 na Abrams ambavyo Ukraine imeviomba, huku Austin akieleza, “tutatoa upya nia yetu ya dhati ya pamoja kuisaidia Ukraine kujilinda kwa kipindi kirefu” katika mkutano wa Ramstein lakini hawakutaja aina maalum ya vifaa vipya.

Zelenskyy ameweka wazi kuwa kile ambacho Ukraine inahitaji ni kupatiwa vifaru vya kisasa. Katika hotuba yake siku ya Alhamisi jioni kwa njia ya video, alisema nchi yake inatarajia “maamuzi makubwa “ na “msaada imara wa kijeshi kutoka Marekani.”

Russia ilisema Ijumaa vifaru vyovyote vya ziada vitakavyopelekwa Ukraine havikuwa na athari yoyote katika mwelekeo huo wa vita.

“Tumerejea kusema kuwa aina hii ya vifaa vinavyopelekwa kimsingi havitabadilisha kitu chochote, lakini vitaongeza matatizo kwa Ukraine na watu wa Ukraine,” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi mjini Moscow.

Alisema nchi za Magharibi “zitajutia imani yake potofu” kuwa Ukraine itashinda katika vita hivi.

Marekani siku ya Alhamisi ilitangaza msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola za bilioni 2.5 ambao haukujumuisha vifaru.

Mwisho..

Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.

XS
SM
MD
LG