Serikali ya Kenya imeeleza kuwa imetoa shilingi bilioni mbili za ziada kuwapa wakenya wapatao laki nane chakula na maji katika majimbo kumi na matatu yanayokabiliwa na baa la njaa.
Takriban majimbo kumi na matatu yamejikuta katika hatari ya kukabiliwa na baa hilo la njaa. Mwandishi wetu anaeleza kuwa maeneo hayo ni Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Marsabit, Wajir, Kilifi, Tana River, Samburu, Makueni, Isiolo, Mandera,Kajiado, Kwale na Garissa. Kati ya haya ni Turkana, Pokot Magharibi na Marsabit ambayo yameathirika zaidi.
Serikali yalaumiwa
Viongozi kutoka majimbo haya wanaeleza kusuasua kwa serikali kuu na zile za majimbo katika kukabiliana na janga hilo la njaa.
Ripoti hizo zimeikumbusha serikali ya Kenya ambayo kuna madai ya kuwa imepuuzilia mbali tishio hilo la njaa na kuzitajia kuwa zenye uvumi tu huku ikisisitiza kuwa havipo viashiria vyovyote vinavyoonesha kuwa Kenya huenda ikajikuta katika hali mbaya zaidi.
James Oduor, Afisa mkuu mtendaji wa halmashauri ya Usimamizi wa Kudhibiti Ukame nchini Kenya anaeleza kuwa vifo hivyo vilisababishwa na maradhi mengineyo.
Serikali yafafanua kuhusu njaa
James Oduor amesema : “Ni kweli vifo vipo lakini ripoti ambayo tumeipata katika maeneo yaliyotajwa haihusishi vifo hivyo na athari ya balaa la njaa. Vifo hivyo vinaoanishwa na maradhi mengine yasiyohusikana na balaa la njaa. Kwa ufahamu wetu hatuna ripoti ya vifo sampuli hiyo.”
Wakati halmashauri hiyo inaeleza kuwa zipo juhudi za kutosha kuondosha hatari kama hiyo, serikali ya Kenya imetangaza mfuko wa ziada wa shilingi bilioni mbili kuwanusuru Wakenya wanaokabiliwa na baa hilo.
William Ruto
Naye Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto baada ya kukutana na mawaziri wanne-Eugene Wamalwa wa Ugatuzi, Mwangi Kiunjuri wa Kilimo, Simon Chelugui wa Maji na Waziri wa Hazina ya Kitaifa Henry Rotich, ameeleza kuwa serikali ya Kenya imekuwa ikiweka mikakati ya kudhibiti ukosefu wa chakula.
Ruto amesema :“Serikali ya Kenya imeamuru kuwasilishwa kwa shilingi bilioni mbili kuanzia wiki hii kutumika kuhakikisha visima vya maji vinajengwa,kupatikana kwa chakula cha kutosha kupitia wizara ya ugatuzi na kufanikisha juhudi za kufikisha chakula hicho kwa watu wanaoathirika kupitia wizara ya kilimo.”
Mlipuko wa magonjwa
Kando na kuwepo kwa uhaba wa mvua nchini Kenya, halmashauri ya usimamizi na udhibiti wa ukame, inaeleza kuwa baa la njaa pia limesababisha magonjwa kwa mifugo, uvamizi wa wadudu mashambani na vile vile kuwepo kwa vita vya ndani kwa ndani kati ya jamii za wafugaji katika maeneo yenye ukame.
Hata hivyo, idara ya utabiri wa hali ya hewa imeeleza kuwa maeneo mengi nchini Kenya, yataanza kupokea mvua mwezi wa Aprili 2019 na hali hiyo inatarajiwa kufuta athari iliyopo ya baa la njaa kufuatia kipindi kirefu cha kiangazi kilichoshuhudiwa maeneo mengi nchini Kenya.
Novemba mwaka jana, serikali ilieleza kuwa shilingi bilioni 167 zitahitajika kutekeleza mpango unaolenga kuwezesha upatikanaji wa chakula cha kutosha kufikia mwaka 2027.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya.