“Hali ya ukame imefikia kiwango cha hatari. Asilimia 80 ya mifugo imekufa na hivi sasa tunajitahidi kuwaokoa watu, ambao pia wameanza kufa. Mpaka sasa, tumerikodi vifo vya watu 25, wengi wao wakiwa watoto wadogo waliokufa kwa njaa,” amesema Ahmed Abdi Salay, gavana wa Somaliland kaskazini magharibi ya mkoa wa Sanag.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watoto 50,000 katika eneo la Somaliland na Somalia wanakabiliwa na balaa la kupoteza maisha kwa sababu ya ukame unaoendelea katika eneo hilo.
Somaliland ilitangaza uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991, lakini haitambuliki na nchi yoyote ile.
Habari kuhusu vifo hivyo katika eneo la Sanag zimetuka siku moja baada ya tovuti ya radio ya serikali ya Mogadishu kuripoti kuwa sio chini ya watu 26 wamekufa kutokana na njaa katika eneo la Kusini mwa Jubaland.
Gavana wa mkoa wa Togdheer katika Somaliland, Mohamud Ali Saleban amesema ukame unaendelea kuathiri katika kila pembe ya jamii ya Wasomali.
Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire alimchagua waziri wa udhibiti wa maafa katika baraza lake la mawaziri, akisema kuwa wizara hiyo itashughulikia na ukame ambao umeacha zaidi ya wasomali milioni 6 wakihitajia msaada.
Gavana Salay amesema zaidi ya watu 15,000 ambao wamekimbia kutoka vijijini sasa wanaishi kwenye kambi za watu waliokimbizwa na vita katika mkoa wa Sanag ambao ni makao makuu ya Erigavo.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama cha madaktari wa Somalia, kikundi cha madaktari wa Mogadishu wameungana na kampeni za kusaidia waliokumbwa na ukame, wakitoa tiba kwa watu katika makambi hayo ya wale waliokimbizwa na vita.