Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 10, 2025 Local time: 05:20

Watanzania watakiwa kuungana kukemea vitendo vya utekaji nchini


Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa ACT Wazalendo. Picha na VOA/ Amri Ramadhani
Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa ACT Wazalendo. Picha na VOA/ Amri Ramadhani

Watanzania wametakiwa kusimama pamoja na kupaza sauti dhidi ya vitendo vya utekaji vinavyoendelea nchini na jeshi la polisi latakiwa kukubali uwepo wa vitendo hivyo na kuwajibika kwa kufanya uchunguzi

Wakizungumza na Sauti ya Amerika wanaharakati na wasoni nchini humo wamevitaka vyombo vya dola kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa ACT Wazalendo Abdul Nondo na muathirika wa vitendo vya utekaji amesema serikali inapaswa kujali usalama wa raia wake kwa kuwa vitendo vya utekaji kwa mwaka 2024 vilikithiri kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Nondo amesema licha ya vitendo hivyo kushamiri, kumekuwa na ukimya kutoka kwenye vyombo vya dola wa kushindwa kutoa taarifa rasmi juu ya uwepo na ukemeaji wa vitendo hivyo.

“Ndugu Watanzania usalama wetu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele kikubwa sana kwani hakuna jambo la thamani zaidi ya uhai na usalama wa raia, na hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha utekaji na mauaji” amesema Nondo

Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utekaji nchini, Nondo amewataka wananchi kupaza sauti na kuishinikiza serikali kuunda tume ya kijaji itakayochunguza matukio hayo ya utekaji, na kufuta kifungu cha sheria kinachotoa ruhusa kwa afisa usalama wa taifa kukamata wananchi pamoja na kuundwa kwa chombo huru cha kiraia kitakachopokea malalamiko ya wananchi dhidi ya jeshi la polisi.

Naye Dkt Paul Loisuilie Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Dodoma anasema licha ya wadau kupaza sauti mara kwa mara kuitaka serikali kushughulikia matukio ya utekaji lakini kumekuwa hakuna utayari wa kisiasa wa serikali iliyopo madarakani kushughulikia changamoto hiyo.

“Tatizo ni kuwa hatuna nia ya kisiasa ya kushughulikia changamoto hii kama tungekuwa na nia ya kisiasa wala haichukui muda, ni suala la muda mchache tu, watu wataandaa utaratibu watazungumza masuala yataisha” amesema Loisuilie.

Hata hivyo Buberwa Kaiza Mchambuzi wa masuala ya siasa amelitaka jeshi la polisi kuweka wazi juu ya uwepo wa vitendo hivyo na kuwajibika kukomesha vitendo hivyo baadala ya kuendelea kuwaficha wananchi.

“Baadala ya Polisi kuficha ukweli huu wa mambo yanayoendelea ya kuteka watu iweke wazi na, yenyewe iyonekana kwamba ipo kazini kushughulikia tatizo hili isionekana kwamba raia peke yao ndiyo wanaohangaika kutatua tatizo wakati vyombo vya usalama vipo” amesema Kaiza

Aidha Kaiza amewataka wananchi kupaza sauti kwa pamoja kuishinikiza serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuja na majibu ambayo yatasaidia kupunguza vitendo vya utekaji, baadala ya kuwaachia jukumu hilo wanaharakati pekee.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG