Wanawake na wasichana wanalazimika kutembea mwendo mrefu wakitafuta maji au kuhudhuria masomo, suala ambalo linawaweka kwenye mazingira hatarishi.
Wakati jua linatua kwenye kambi ya wakimbizi ya Adan Saleban yenye watu walioathiriwa na ukame kwenye eneo la Somaliland, kumbukumbu zinampata mama wa watoto 6 mwenye umri wa miaka 35.
Novemba wakati mume wake alipokuwa kitandani kutokana na ugonjwa, mwanamme mmoja alimvamia nyumbani kwake na kumbaka wakati alipokuwa akiwalaza watoto wake.
Yeye hataki kutumia jina lake kamili kwa kuhofia unyanyapaa.
Muathirika wa ubakaji anaeleza: Taa ya kandili ilikuwa inawaka na hivyo mwanamme huyo aliweza kuniona kwa urahisi na mara moja alianza kurarua nguo zangu. Nilijaribu kushindana naye lakini alinishinda nguvu. Majirani walifika ili kunisaidia baada ya kupiga mayowe, lakini tayari mtu huyo alikuwa amekimbia.
Visa kama hivyo ni vya kawaida kwenye kambi hiyo inayotoa hifadhi kwa zaidi ya familia 2,000.
Wanawake kadhaa na wasichana katika kambi hiyo walizungumza na mwanahabari wakitaka kusimulia hadithi zao kuhusu kushambuliwa au hofu waliyo nayo kwa ajili ya watoto wao.
Wafanyakazi wa misaada wamethibitisha kuwepo kwa visa vya ukatili wa kijinsia.
Kliniki inayotoa huduma za afya au ushauri nasaha kwa manusura iko umbali wa takriban kilomita 100.
Kliniki hiyo ya Ainabo inasema kwamba visa vya ukatili wa kijinsia vimeongezeka mara nne tangu ukame ulipoingia, na kufikia takriban visa 20 kila mwezi, lakini vingi haviripotiwi kutokana na hofu ya unyanyapaa.
Rahma Saidi mfanyakazi katika kliniki hiyo ya Ainabo anayhusika na masuala ya ukatili wa kijinsia anaelezea.
Rahma, "Sisi huwa tunawapa msaada wa kisaikolojia na iwapo wanahitaji msaada wa kisheria, sisi huwatuma kwa watalaam wa sheria."
Wafanyakazi wa misaada wanasema kwamba hali iliyopo imefanya kuwa vigumu kwa wasichana kuhudhuria masomo.
Khadija Qulle pamoja na binti zake wanne vijana wamekuwa kwenye kambi ya Adan Saleban tangu Machi baada ya ukame kuuwa mifugo yao. Anasema kwamba mume wake alikufa kutokana na msongo wa mawazo.
Qulle alilazimika kuwaondoa binti zake kutoka kwenye shule iliyoko takriban kilomita 5 kutoka kwenye kambi hiyo, kwa kuhofia usalama wao wakati wakitembea ili kuhudhuria masomo.
Shirika la kutoa misaada ya CARE Somalia linasema kwamba kuna watoto 900,000 waliokoseshwa makazi, ambao wapo kwenye hatari ya kuacha shule, 43,000 miongoni mwao wakiwa kwenye kambi za wakimbizi za Somaliland.
Mamlaka zinasema kwamba zinajaribu kuimarisha usalama, lakini inakuwa vigumu kwa kambi kama ya Adan Salbean kutokana na umbali wake pamoja na ukosefu wa umeme. Jua linapotua wanawake na wasicaha ambao tayari wameathiriwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea ndani ya miaka 50, pia wanahofia hatari za aina nyingine zinazoweza kutokea nyakati za usiku.