Lakini licha ya janga hili kuna mazuri ambayo yalitokea na mengine kuwatia hamasa kubwa wanawake duniani kuwa wanaweza kufanya mengi katika kuleta mabadiliko katika jamii na taifa.
Kwa mara ya kwanza katika siasa za Marekani tumeshuhudia historia ikiandikwa na mwanamke wa kwanza mweusi mwenye asili ya Asia ambaye alichaguliwa kushika wadhifa wa juu wa uongozi katika taifa la Marekani.
Makamu rais mteule Kamala Harrsi alichaguliwa na rais mteule Joe Biden kuwa mgombea mwenza wake katika tiketi ya chama cha Democratic kuwania urais wa Marekani katika uchaguzi wa November 3. Na historia itaandikwa hapo Januari 20 wakati rais mteule Joe Biden atakapoapishwa na kushika rasmi hatamu za uongozi.
Nako nchini Tanzania mwaka huu tumeona idadi kubwa ya wanawake waliingia katiika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi mkuu na kubainisha kuwa wanawake wanapoamua wanaweza.
Aliyekuwa mgombea urais Queen Cuthbert Sendiga wa chama ADC amesema kuwa wakati umefika kwa wanawake kuwania nafasi za uongozi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Na sasa basi tuelekee katika maeneo mengine huko Afrika tukianzia nchini Misri ambako mwaka huu lilianzishwa rasmi Jukwaa la Sauti Milioni 50 Afrika.
Lakini hatuwezi kusahau jinsi janga la Covid 19 lilivyochangia kubadili hali ya maisha ya wanawake huko Afrika Mashariki hasa kutokana na kuwekwa kwa masharti mbali mbali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Mataifa yote ya Afrika Mashariki na Kati yana hadithi inayofanana kuhusu janga la Covid 19 na changamoto mbali mbali ambazo wamekabiliana nazo wanawake katika kuendesha shughuli zao za kila siku.
Lakini licha ya janga la Covid 19 wanawake wa Congo nao walikuwa na simanzi kwa kuvuliwa uspika wa bunge kwa mwanamke ambaye wanasema alikuwa tumaini lao.
Hali haikuwa tofauti katika nchi za Rwanda, Uganda na Burundi kwani wanawake pia katika nchi hizo walishuhudia kukumbwa na changamoto zisizo za kawaida ili kuwa katika hali ya kuona kuwa wanamudu kujikimu kimaisha ili kuhudumia familia na wakati huo huo kuepukana na matatizo ya janga la corona.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Khadija Riyami kwa niaba ya waandishi wa VOA Salma Mohamed, Mombasa, Kenya , Shafii Mbinda kutoka Cairo, Misri na Austere Malivika Goma, DRC