Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:18

Biden akubali rasmi uteuzi wa chama kugombea urais wa Marekani


Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden akitoa hotuba ya kukubali rasmi uteuzi wa Chama cha Demokratik kugombea urais wa Marekani akiwa mjini Wilmington, Delaware. Agosti 21, 2020.
Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden akitoa hotuba ya kukubali rasmi uteuzi wa Chama cha Demokratik kugombea urais wa Marekani akiwa mjini Wilmington, Delaware. Agosti 21, 2020.

Makamu rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, hatimaye Alhamisi alikubali rasmi uteuzi wa chama cha Democratik kuwa mgombea wa urais Marekani .

Katika hotuba ambayo aliitumia kutoa mtazamo wake kwa nchi akitafuta uungwaji mkono katika juhudi zake za kutaka kumshinda Rais Donald trump katika uchaguzi mkuu wa Novemba tatu mwaka huu, Biden aidha aliukosoa utendakazi wa Rais Trump na kusema kwamba iwapo atachaguliwa, ataubadilisha mstakabal wa Marekani.

Alimtaja Trump kuwa mtu ambaye hawajibiki katika kukabiliana na janga la Corona na kwamba "anakataa kuongoza."

"Kwa pamoja tunaweza na tutaweza kuibuka kutoka kipindi hiki cha giza," alisema mwanasiasa huyo mkongwe, mwenye umri wa miaka 77.

Hotuba ya Biden, ambayo iliangazia masuala mengine kadhaa, kwenye usiku wa nne na wa mwisho wa mkutano mkuu wa chama cha Democratik, aliitoa akiwa katika mji anaotoka wa Wilmington kwenye jimbo la Delaware, hata ingawa awali chama cha Demokratik kilikuwa kimepanga hafla hiyo ifanyika mjini Milwaukee, Wisconsin.

Hotuba hiyo imetajwa na wachambuzi kama iliyo muhimu zaidi kwa maisha yake yote ya kisisa.

Hii na baada ya takribani miaka 50 ya kuhudumu afisi za umma na kujaribu mara mbili mawili kuingia White House - mwaka 1988 na 2008- lakini akashindwa.

"Hajawahi kukaribia kiti cha urais jinsi hii katika maisha yake yote. Bila shaka anayo nafasi nzuri mwaka huu," alisema Profesa David Monda, Mhadhiri wa chuo kikuu cha New York na mchambuzi wa masuala ya siasa.

Biden alimteua Seneta wa jimbo la California Kamala Harris kama mgombea mwenza, amabye alikubali rasmi uteuzi huo Jumatano usiku.

Makamu Rais wa zamani Biden, mkewe Jill Biden, Seneta Kamala Harris na mmewe, Doglas Emhoff
Makamu Rais wa zamani Biden, mkewe Jill Biden, Seneta Kamala Harris na mmewe, Doglas Emhoff

Kabla ya Biden kuhutubia wafuasi wake, wademokrat wa ngazi ya juu walitoa hotuba zao, wakiwemo Seneta Cory Booker na meya Pete Bittigieg.

Mkutano huo uliomalizika Alhamisi ulifanyika kwa kiasi kikubwa kwa njia ya kimtandao, na ulihudhuriwa na wazungumzaji wakiwemo baadhi ya viongozi wa vyeo vya juu katika chama hicho na hata Warepublican maarufu, ambao walimsifia Biden katika hotuba za video na kutoa wito wa haraka kwa wapiga kura kumaliza "mgawanyiko ulioletwa katika urais wa Trump."

Lakini Rais Trump, akizungumza Alhamisi katika mji wa Old Forge jimbo la Pennsylvania, aliwaambia wafuasi wake kwamba Biden hawezi kuiongoza vyema Marekani.

"Mkitaka kujua vile urais wa Biden unaweza kuwa, tazameni mabaki yanayotoka moshi mjini Minneapolis, vurugu mjini Portland na barabara zilizojaa damu mjini Chicago, kisha fikirieni ghasia zitakazokuwa kwa kila mji wa Marekani," alisema kabla ya Biden kutoa hotuba yake.

Chama cha Republikan kinatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi wiki ijayo, ambapo Trump na makamu wake, Mike Pence, watakubali rasmi uteuzi wa chama hicho.

XS
SM
MD
LG