Kauli mbiu ya mwaka 2020 ni kila mtu ni haki sawa, ikimaanisha kuwa hiyo ni kuelekea katika kuiwezesha dunia, na pia kusherehekea mafanikio ya wanawake na kuhakikisha kuwa hatua zinachukuliwa kwa ajili ya usawa kwa wote.
Umoja wa Mataifa uliridhia kuadhimishwa rasmi siku ya kimataifa ya wanawake March 8 mwaka 1975 kwa lengo la kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia. Uamuzi huu ulifikiwa kupingana na mfumo dume ambao ulitamalaki katika jamii mbali mbali kote ulimwenguni na kuminya haki za msingi za wanawake.
Tangu wakati huo tumeshuhudia mafanikio mengi yametokea kwa upande wa wanawake barani Afrika hasa katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Siyo tu katika nyaja ya kiuchumi na kisiasa lakini pia katika elimu na masuala ya kijamii kama vile kuhamasisha kupiga marufuku mila potofu ambazo zinamkandamiza mtoto wa wa kike, kama vile ukeketaji, ndoa za mapema na mtoto wa kike kuwa katika nafasi ya mwisho baada ya fursa zote za elimu kupewa mtoto wa kiume katika jamii.
Moja ya mafanikio makubwa sana ambayo wanawake wanajivunia kupatikana katika suala zima la haki sawa kwa wote ni wao kupewa sauti na fursa ya kufanya maamuzi kuzungumzia na kusuluhisha mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika sekta mbali mbali. Kuanzia vita na mizozo mpaka manyanyaso ya kijinsia.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Khadija Riyami, Washington, DC.