Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 03, 2025 Local time: 02:23

Wagonjwa washindwa kupata matibabu kufuatia mgomo wa madaktari Kenya


Wanafunzi wa udaktari wakifanya mgomo nje ya hospitali ya kenyatta huko Nairobi Julai 14, 2021. Picha na Patrick Meinhardt / AFP
Wanafunzi wa udaktari wakifanya mgomo nje ya hospitali ya kenyatta huko Nairobi Julai 14, 2021. Picha na Patrick Meinhardt / AFP

Wagonjwa wamekwama katika hospitali mbalimbali nchini Kenya kufuatia mgomo wa madaktari unaolenga kuwezesha utekelezaji wa mahitaji ya nafasi za lazima za mafunzo ya utabibu kwa zaidi ya madaktari waliohitimu 4,000, ajira na mazingira bora ya kazi.

Madktari katika mgomo huo ulioanza siku ya Alhamisi, pia wanadai kurejeshewa ushuru wa nyumba uliokatwa katika mishahara yao, kucheleweshwa kulipwa mishahara na kushindwa kuwasilisha makato ya kisheria pamoja na utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya na kuwahakikishia madaktari wanaotoa huduma chini ya mpango wa afya kwa wote kuajiriwa kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya pamoja ya 2017.

Dkt Davji Atellah, Katibu mkuu wa Muungano wa madaktari nchini Kenya, KMPDU ameiambia Sauti ya Amerika, kuwa mgomo huo utaendelea hadi serikali itakapoonyesha nia ya kutekeleza matakwa ya mgomo huo.

Mbali na serikali kusema haina bajeti ya kutekeleza masharti hayo, mahakama Jumatano, ikisitisha mgomo huo, na kuwataka madaktari na serikali kufanya mazungumzo ya kufuta utata uliopo kwa haraka, kupitia mazungumzo yenye tija.

Wafanyakazi wa afya wamekusanyika nje ya wizara ya Afya ya Kenya ili kudai nyongeza za mishahara na mazingira bora ya kazi.
Wafanyakazi wa afya wamekusanyika nje ya wizara ya Afya ya Kenya ili kudai nyongeza za mishahara na mazingira bora ya kazi.

Kufuatia mgomo huo siku ya Alhamisi, wagonjwa walishindwa kupata matibabu kutoka katika vituo cha afya vya umma na kulazimika kutafuta huduma hizo kwenye zahanati binafsi.

Baadhi ya hospitali ambazo hazikuathirika na mgomo huo, zilipokea viwango vya chini vya huduma za afya, baada ya madaktari kususia kazi kama ilivyoshuhudiwa mjini Mombasa.

Akizumgumza na waandishi wa habari huko Mombasa, Dkt Atellah amesema kuwa serikali imekuwa ikifanya mazungumzo ya mara kwa mara na madaktari yasiokuwa na suluhu, na huu ndio wakati wa kutimiza ahadi ya utekelezaji wa mkataba wa pamoja wa mwaka 2017.

Kwa muda sasa utekelezaji wa mkataba wa makubaliano wa 2017-2021 ulioazimia kutatua uhaba wa madaktari, kuweka nyongeza ya mishahara na kuimarisha mazingira ya kazi, kuwapandisha madaktari vyeo na kupatikana kwa vifaa hitajika vya matibabu, na utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya umesababisha zogo hili kutokana na kigugumizi cha serikali kuutekeleza.

Mara kadhaa, madaktari nchini Kenya wamelalamikia kiasi cha nyongeza ya mshahara wa kiwango cha chini, utatuzi wa suala la uchelewashaji wa malipo ya mishahara na marupurupu kwa madaktari, makato ya pesa yasiolipwa kisheria na malipo ya bima, bima ya matibabu kwa madaktari wote, kuajiriwa kwa madaktari wasiokuwa na kazi rasmi, ukosefu wa vifaa hitajika kazini, mafunzo ya baada ya kuhitimu na kupandishwa cheo kwa madaktari, mikopo ya magari na rehani za nyumba, pamoja na ajira ya madaktari kwa masharti ya kudumu na pensheni.

Ripoti hii imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika

Forum

XS
SM
MD
LG