Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa adhabu hiyo ni faini ya jumla ya shilingi milioni 60 kwa televisheni hizo binafsi kwa madai ya kukiuka kanuni za utangazaji .
Vituo hivyo vinatuhumiwa kuripoti utafiti uliofanywa na kituo cha sheria na haki za binadamu kuhusiana na uchaguzi wa madiwani uliofanyika hivi karibuni katika kata 43 nchini.
Televisheni hizo zilidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi ya nguvu za dola pamoja na wafuasi wa vyama kuumizana
Kwa mujibu wa Yahya Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kituo cha televisheni cha AzaM cha jijini Dar es salaam ambacho ni miongoni mwa waliokumbwa na adhabu hiyo ya faini, wanatambua umuhimu wa kuzingatia weledi katika uandishi wa habari, lakini sheria zinazotumika zinaweza zisisaidie vyombo hivyo kukua
Aidha VOA ilizungumza na Mwandishi mwandamizi wa kituo cha Channel Ten Kibwana Dachi, ambacho pia kimeadhibiwa kwa faini ya shilingi milioni 15, ambaye anasema serikali ilipaswa kikihoji au kukiadhibu kituo cha sheria na haki za binadamu ambacho ndicho kilitoa hizo tafiti za uchaguzi wa madiwani kama kulikuwa na tatizo walilodai la uchochezi.
Kwa upande wake Afisa wa Programu wa Baraza la habari Tanzania (MCT) Pili Mtambalike ametaka waandishi wa habari kupigania kuondokana na sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari ambazo zikitumika zinaweza kuwa na athari katika maendeleo ya taaluma ya habari.
Vituo binafsi vilivyopigwa faini ni pamoja na ITV, Channel Ten na East Africa ambao wamepigwa faini ya shilingi milioni 15 kila kituo huku Star TV, na Azam TV wakitakiwa kulipa milioni 7.5 kila kituoambao wanatakiwa kulipa adhabu hiyo ndani ya siku thelathini kuanzia January 2 mwaka huu