Kudidimia kwa maadili
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa hali hiyo imepelekea kuonekana kuwa kuna udidimizaji wa maadili na sheria zinazotungwa na hivyo wenyewe kwa wenyewe wameendelea kukumbushana kuziheshimu sheria hizo wakati wanapojadili masuala ya nchi.
Shutuma hizi zimetokea chini ya kipindi cha wiki moja, baada ya bunge la Kenya kuripotiwa na gazeti moja nchini kwa madai ya kuwa wabunge hupokea rushwa ili kuidhinisha au kutoidhinisha ripoti za kamati za bunge.
Pia inadaiwa kuwa rushwa hutumika ili kuwafanya wabunge wawakingie kifua watu mashuhuri serikalini ili kuwaondoa kwenye lawama.
Mjadala bungeni
Alhamisi iliyopita wakati wabunge wakijadili ripoti inayochunguza jinsi sukari inayokisiwa kuwa na madini ya zebaki na shaba ilivyoingizwa Kenya, wabunge wengi walitofautiana juu ya ripoti inayowalimbikizia lawama waziri wa hazina ya kitaifa Henry Rotich, Adan Mohamed mmiliki wa viwanda na aliyekuwa Waziri wa kilimo Willy Bett kwa kuonyesha utepetevu kazini na kutaka wachunguzwe.
Mwandishi wetu ameripoti kuwa nyuma ya sauti nyingi za kutupilia mbali ripoti hii palikuwepo mkono wa mawakala waliotumwa na kupewa masharti ya kufanikisha juhudi za kutoiidhinisha ripoti hiyo.
Madai dhidi ya wabunge
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amedai kuwa mbunge wa kaunti ya Wajir Fatuma Gedi alimkabidhi kitita cha fedha akimtaka asiiidhinishe ripoti hiyo.
Pia kuna madai ya kuwa baadhi ya wabunge walioitupilia mbali ripoti hii walikuwa wamepewa kati ya shilingi elfu kumi na elfu thelathini, ili mawaziri hawa waliotajwa katika ripoti hii wasije kufikwa na mkono wa sheria au hata kufikwa na hoja ya kutokuwa na imani nao.
Pia kuna madai ya kuwa wabunge walijikusanya katika makundi kadha kuwatetea viongozi mawaziri wanaotoka katika maeneo yao.
Hilo lilipowaafiki, waliitupilia mbali ripoti hii kwa kauli moja. Mbunga Kanini Kega, mwenyekiti wa kamati ya bunge iliyotayarisha ripoti hii akieleza kutamaushwa kwake.
Hata hivyo, mbunge wa jimbo la Wajir, Fatuma Gedi anayeshtumiwa kuwagawia wabunge fedha kutoiidhinisha ripoti hii amekana madai hayo.
"Ni suala ambalo umma unalijua kwamba wanakamati hawa walibadilishwa mawazo. Mimi binafsi sikumpa mbunge yeyote mlungula. Siwezi kumhonga mbunge na shilingi elfu kumi pekee. Hiyo ni kudhalilisha wabunge," amesema Gedi.
Kauli ya spika wa bunge
Spika wa bunge Justin Muturi sasa anaitaka tume ya kupambana na ufisadi (EACC) kuingilia kati.
Idara husika za uchunguzi na kupambana na ufisadi zimeongeza juhudi za kuwashtaki maafisa wanaotajwa katika mtego wa ufisadi na vile vile kuchunguza uozo kwenye nyumba ya waheshimiwa.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika VOA, Nairobi.