Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:32

Kenyatta kuzuru White House kwa mwaliko wa Trump


Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (Kushoto) asalimiana na Rais Donald Trump wa Marekani walipohudhuria mkutano wa G7 nchini Italia tarehe 27 mwezi Mei, 2017. Mkewe Trump, Melania Trump (Kulia), anawatazama.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (Kushoto) asalimiana na Rais Donald Trump wa Marekani walipohudhuria mkutano wa G7 nchini Italia tarehe 27 mwezi Mei, 2017. Mkewe Trump, Melania Trump (Kulia), anawatazama.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, atazuru White House mwishoni mwa mwezi huu kwa mwaliko wa rais wa Marekani, Donald Trump.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisi ya mawasiliano ya White House Jumatatu, katika mkutano huo, marais hao wawili watakutana tarehe 27 mwezi huu na kuangazia mikakati ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

"Mkutano huo utasisitiza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Marekani na Kenya kama nguzo muhimu ya amani na utulivu, siyo tu barani Afrika, ila pia katika eneo nzima linalozungukwa na bahari Hindi," taarifa hiyo ilisema.

"Rais Trump na Rais Kenyatta watajadili njia za kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili, pamoja na ushirikiano katika nyanja ya usalama," iliongeza taarifa hiyo.

Msemaji wa ikulu ya Nairobi, Kanze Dena alithibitisha kwamba Kenyatta aliupokea mwaliko huo na kwamba atafanya ziara rasmi mjini Washington mwishoni mwa mwezi huu.

Kenyatta atakuwa rais wa pili wa nchi za Afrika chini ya jangwa la Sahara kualikwa White House na wa tatu katika bara lote.

Marais wa Misri, Abdel el Sisi na yule wa Nigeria, Muhamadu Buhari tayari wamezuru ikulu ya Washington kwa mwaliko wa Trump.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Prof Fulbert Namwamba, aliiambia Sauti ya Amerika Jumatatu kwamba rais Trump ananuia kuonyesha kwamba anatambua umuhimu wa Kenya katika eneo linalozingira bahari Hindi.

"Kama tunavyojua, Trump hajaonyesha shauku kubwa kwa masuala ya Afrika, lakini pia anajua kwamba Kenya ni muhimu mno hususan katika vita dhidi ya ugaidi," alisema Namwamba kwa njia ya simu.

"Hiyo bila shaka ndiyo sababu moja muhimu iliyopelekea uamuzi wa Trump katika suala hili la kutoa mwaliko," aliongeza.

Ziara ya Kenyatta inajiri huku baadhi ya wachambuzi wakisema kuwa tofauti na ilivyokuwa awali, utawala wake umeegemea zaidi kwa upande wa China kwa mikopo ya kugharamia miradi mikuu inayotekelezwa na serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Marekani imekuwa ikiishinikiza Kenya kuongeza juhudi zake katika vita dhidi ya ufisadi na utawala wa Trump umeahidi kwendelea kutoa usaidizi wa kupambana nao.

Trump walikutana mara ya mwisho na Kenyatta tarehe 27 Mei, 2017 nchini Italia, wakati wa kongamano la kilele la mataifa saba tajiri zaidi duniani (G7) ambapo alikuwa amealikwa pamoja na viongozi wa Ethiopia na Nigeria.

XS
SM
MD
LG