Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 09:57

Viongozi wa Marekani wawarai wabunge kupitisha makubaliano ya deni la taifa


FILE - Spika wa Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy wa Calif., kushoto, akisikiliza wakati Rais Joe Biden akiongea kuhusu kikomo cha deni katika ofisi ya Oval, ikulu ya Marekani Mei 29, 2023, mjini Washington.
FILE - Spika wa Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy wa Calif., kushoto, akisikiliza wakati Rais Joe Biden akiongea kuhusu kikomo cha deni katika ofisi ya Oval, ikulu ya Marekani Mei 29, 2023, mjini Washington.

Wabunge wa Marekani wanatathmini maelezo ya makubaliano ya  kuongeza kiwango cha kukopa  kabla ya upigaji kura unaotarajiwa kufanyika siku zijazo, wakati Rais Joe Biden na Spika wa Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy wakiwasihi kuidhinisha hayo makubaliano.

Pendekezo hilo linajumuisha kuondoa ukomo wa deni hadi Januari mwaka 2025 na makubaliano ya bajeti ya miaka miwili itakayowezesha matumizi ya serikali kuu mwaka 2024 na kuongeza matumizi kwa asilimia 1 ifikapo 2025.

Miongoni mwa sehemu nyingine ambazo zilikubaliwa katika mkataba huo ni kupunguza ruzuku ya kuajiri wafanyakazi wa Huduma ya Idara ya Mapato, kufuta msaada wa dola bilioni 30 kwa ajili ya COVID-19 ili kuwahakikishia watu wenye umri wa miaka 49 hadi 54 wanakidhi viwango vya kufanya kazi ili kuweza kupatiwa msaada wa chakula.

Biden na McCarthy walifikia makubaliano Jumapili baada ya wiki kadhaa za mashauriano huku mwanzoni mwa mwezi Juni ndiyo muda wa mwisho ambapo serikali kuu inaweza kuishiwa na fedha za madeni yake.

“Makubaliano hayo yanazuia uwezekano wa kutokea mgogoro, kushindwa kulipa madeni, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya taifa letu,” Biden alisema akiwa White House. Hilo “linaondoa tishio la janga la kutolipa deni kutoka kwenye meza ya mazungumzo.”

McCarthy, akijadili kuhusu mkataba huo huko Capitol, alisema, “Mwisho wa siku, watu wanaweza kuliangalia pamoja ili kuweza kupitisha hili.”

FILE - Rais Joe Biden, kulia alipokutana na Spika Kevin McCarthy kujadili ukomo wa deni taifa , White House, Washington Mei 22, 2023. (AP Photo/Alex Brandon)
FILE - Rais Joe Biden, kulia alipokutana na Spika Kevin McCarthy kujadili ukomo wa deni taifa , White House, Washington Mei 22, 2023. (AP Photo/Alex Brandon)

Wakati viongozi hao wawili wakieleza kuunga mkono makubaliano hayo, wabunge Wademokrat wenye kupenda maendeleo kutoka mrengo wa kushoto wa chama hicho, na Warepublikan kutoka mrengo wa kulia mara moja walielezea upinzani wao Jumapili.

“Mkataba huu unawakilisha kufikia maridhiano, ikimaanisha kuwa siyo kila mtu atapata kile wanachokitaka.

Lakini hilo ndiyo jukumu la utawala,” Biden alisema katika taarifa yake.

Aliuita mkataba huo “ ni hatua muhimu ya kusonga mbele ambayo inapunguza matumizi wakati ikilinda programu nyeti kwa wafanyakazi na kukuza uchumi kwa kila mtu.”

Mapema Jumapili, McCarthy, akizungumza katika kipindi cha “Fox News Sunday”, alisema kuwa mtizamo wa Warepublikan, “Kuna mengi ndani ya mkataba huu ambayo ni mazuri.

Hauwezi kutatua kila kitu kwa kila mtu, lakini hii ni hatua yenye mwelekeo sahihi.

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen

Ukomo wa deni unahitaji kuongezwa ili serikali iweze kukopa fedha zaidi, au serikali ya Marekani itaishiwa na fedha taslimu kulipa bili zake ifikapo Juni 5, Waziri wa Fedha Janet Yellen amelitahadharisha Bunge.

Yellen amesema kuwa bila ya kuongeza ukomo wa deni au kusitisha kiwango cha ukopaji, riba ya dhamana za Marekani zinazoshikiliwa na serikali za nje na wawekezaji binafsi wa Marekani zitakuwa hatarini, hali kadhalika malipo ya wastaafu ya pesheni na mishahara ya wafanyakazi wa serikali na walioajiriwa kwa mikataba.

Bila ya serikali ya Marekani kuwa inapokea kodi ya kutosha kulipa bili zake, serikali italazimika kuweka vipaumbele kuchagua ni malipo yepi yafanyike.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya came AP, AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG