Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 05:22

Viongozi wa dunia walaani Russia kuvamia Ukraine


Vladimir Putin
Vladimir Putin

Huku viongozi wa dunia wakilaani uvamizi huo na kutafuta njia za kukabiliana na mzozo huu ambao haujashuhudiwa kwa karibu miaka 80 sasa.

Macho yote ya dunia Alhamisi yameelekea nchini Ukraine ambako hatimaye Russia imeanza mashambulizi ya ardhi, anga na bahari dhidi ya miji mbali mbali ya taifa hilo.

Huku viongozi wa dunia wakilaani uvamizi huo na kutafuta njia za kukabiliana na mzozo huu ambao haujashuhudiwa kwa karibu miaka 80 sasa.

Rais wa Ukraine ametoa wito kwa wananchi wake kujitayarisha kulilinda taifa lao na kutoa wito kwa viongozi wa dunia kuingilia kati kuzuia uvamizi wa Russia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

Juhudi za wiki kadhaa za kidiplomasia kujaribu kumzuia Rais Vladimir Putin kutekeleza azma yake ya kuivamia Ukraine zimeshindikana baada ya kiongozi huyo kuamuru operesheni maalum ya kijeshi, kupitia nchi kavu, bahari na anga dhidi ya Ukraine.

Mtu yeyote atakaejaribu kutuzuia na kusababisha vitisho zaidi dhidi ya nchi yetu, wananchi wetu wanabidi kufahamu kwamba jibu la Russia litakuwa la haraka na kusababisha athari ambazo hujawhi kushuhudia katika historia yako,” amesema Rais Putin.

Makombora na mizinga imefyetuliwa dhidi ya miji mbali mbali na kulingana na ripoti za vyombo vya habari takriban wanajeshi 40 wa Ukraine wameuliwa pamoja na raia.

Rais Volodymyr Zelensky amelihutubia taifa ameomba amani idumishwe na kusema anavunja uhusiano na Russia na kuwataka wananchi kulilinga taifa lao.

Rais Zelensky alitangaza “asubuhi ya leo ni siku inayoingia katika historia, kwa nchi yetu na Russia. Tunavunja uhusiano wetu na Moscow. Ukraine inajitetea na haitokubali kamwe kushindwa na kupokonywa uhuru wake, bila ya kujali kile Moscow inachokifikiria.”

Mikutano ya dharura inafanyika kila pembe ya dunia ikiwa ni pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, makao makuu ya NATO na Umoja wa Ulaya.

Rais Joe Biden akiungana na viongozi wengine wa dunia wanalaani uvamizi huo wakisema ni kitendo cha vita.

Katika ujumbe wake wa Tweeter Jumatano usiku Biden amesema dunia nzima iko pamoja na wananchi wa Ukraine. Akiongeza kwamba atakutana na viongozi wenzake wa kundi la G7 na kuwahutubia tena wananchi wa Marekani juu ya adhabu kali ambazo Marekani na washirika wake watazichukua dhidi ya Russia.

Joe Biden -U.S. President / Ukraine/ Russia/
Joe Biden -U.S. President / Ukraine/ Russia/

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana kwa kikao nadra cha dharura Jumatano usiku na kulaani vikali uvamizi unaofanywa na Russia bila ya kuchokozwa wala sababu yoyote.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema dunia itajibu kwa pamoja dhidi ya kitendo cha Russia.

“Leo ni siku mbaya kwa Ukraine na misingi ya Umoja wa Mataifa. Baraza hili lazima lichukue hatua na tutawasilisha pendekezo la azimio la kulaani jambo hili. Kama vile Rais Biden alivyosema leo usiku, Russia pekee ndio inawajibika na vifo na uharibifu kutokana na shambulizi hili na Marekani na washirika wake watatoa jibu la pamoja na la nguvu,” amesema balozi Thomas-Greenfield.

China imekataa kuilaani Russia kutokana na uvamizi huo ikisema inafuatilia kwa karibu hali ya mambo ikitoa wito kwa pande zote kustahmiliana.

Waatalamu wa kijeshi wanaripoti kwamba jeshi la Ukraine linajibu vikali mashambulizi hayo wakati wanajeshi wa Russia wakionekana wakifanya mashambulizi bila ya mpangilio maalum kama inavyotarajiwa na jeshi lenye nguvu kama lao.

Waukraine wameshtushwa na uvamizi ambao hawakuamini utatokea na kwa wakati huu maelfu ya watu wanaonekana wakikimbia kutoka mji mkuu wa Kiyv na miji mingine. Picha za vyombo mbali mbali vya habari pia zinaonyesha wananchi wakisimama mbele ya mabenki kuchukua fedha.

Huku milio ya makombora na mizinga ikisikika sehemu mbali mbali ya nchi hiyo.

Wananchi wa Russia kwa upande wao wameshtushwa na wamegawanyika kutokana na uvamizi huo, wengi hata hivyo wakitoa wito wa amani kudumishwa.

XS
SM
MD
LG