Katika hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni, Putin alitangaza kuanza kwa operesheni za kijeshi mashariki mwa Ukraine, ikiwa ni majibu kwa kile alichokiita vitisho vya Ukraine.
Alisema kwamba wale wanaopinga hatua hiyo katika mkoa wa Donbas, watakabiliwa na matokeo ambayo hawajawahi kuyaona.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, alisema wanajeshi wa Russia wamefanya mashambulizi dhidi ya mfumo wa kijeshi wa Ukraine na walinzi wa mpakani.
Alisema serikali itapitisha sheria ya kijeshi kote nchini humo, huku akiwasihi watu wake kuwa watulivu na kubaki majumbani mwao.
Jeshi la Ukraine limesema kwamba Russia ilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ukraine mashariki mwa nchi mapema alhamisi, na imetekeleza mashambulizi ya roketi kwenye viwanja vya ndege katika miji mbalimbali kote Ukraine.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema kwamba watu wa Ukraine wanataabika kutokana na uchokozi usiokuwa na sababu, kutoka kwa wanajeshi wa Russia na kwamba Russia itawajibishwa.