Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 10:49

Vijana wa Tanzania watakiwa kuwa wabunifu katika utalii


Wafanyakazi wa scuba diving huko Zanzibar. Picha Picha na Sumy Sadurni / AFP.
Wafanyakazi wa scuba diving huko Zanzibar. Picha Picha na Sumy Sadurni / AFP.

Wakati Dunia ikiadhimisha siku ya utalii Duniani vijana nchini Tanzania wametakiwa kuwa wabunifu ili kuendana na ukuaji wa sekta ya utalii na kuwawezesha kujipatia ajira kupitia ubunifu unaoendana na mahitaji ya utalii nchini.

Huku wadau wa utalii nchini humo wakiitaka serikali kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara zinazioelekea kwenye vivutio vya utalii ili kurahisisha shughuli za utalii na kuchochea ukuaji wake.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inakuwa kwa kasi katika sekta ya utalii barani Afrika, huku sekta hiyo ya utalii ikichangia sehemu kubwa ya pato la taifa na kutoa ajira kwa idadi kubwa ya wananchi nchini humo.

Licha ya ukuaji huo bado sekta ya utalii nchini Tanzania imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa hoteli katika baadhi ya vivutio hali inayopelekea usumbufu kwa watalii wakati ambao panakuwa na idadi kubwa ya watalii kama anavyoeleza Akizungumza na Sauti ya Amerika, Jonasi Ndunguru ambaye ni mmiliki wa kampuni ya utalii inayojulikana kama Joagro Safaris Tanzania amesema,

Watalii wakiwa katika mbuga ya wanyama ya Serengeti, Tanzania.
Watalii wakiwa katika mbuga ya wanyama ya Serengeti, Tanzania.

“Katika miezi ambayo tunakuwa na watalii wengi tunatafuta hoteli sehemu mbalimbali lakini unakuta hoteli hakuna ambayo hii inasababishwa na ongezeko kubwa la watalii nchini” amesema Ndunguru.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la utalii Duniani inayojulikana kama “Travel and Tourism: Economic Impact Research 2024,” imeonyesha kuwa Tanzania kwa mwaka 2023 imeingiza Tsh Trillion 18.6 kupitia utalii na safari ikiwa ni rekodi kubwa ya mapato kuwahi kutokea.

Baadhi ya wamiliki wa makampuni ya usafirishaji watalii wameeleza kuendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu bora ya barabara zinazoelekea katika mbuga za wanyama kama anavyoeleza Kelvin Nasari mmiliki wa kampuni ya usafirishaji wa watalii inayojulikana kama Tanzania Safari Operation Limited.

“Barabara kuelekea kwenye vivutio vyetu vya utalii hasa katika mbuga za wanyama imekuwa ni changamoto sana barabara ni mbovu inatuchosha sisi kama wasafirishaji wa watalii na hata watalii wenyewe wanachoka” amesema Nasari.

Ripoti hiyo ya Baraza la utalii Duniani inaendelea kueleza kuwa ajira katika sekta ya utalii Tanzania kwa mwaka 2023 zilifikia watu milioni 1.4 ikiwa ni ongezeko la ajira 97,000 lakini zikiwa pungufu kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa na rekodi ya juu ya mwaka 2019.

KUndi la tembo likiwa katika mbuga ya wanyaza ya Serengeti, Tanzania.
KUndi la tembo likiwa katika mbuga ya wanyaza ya Serengeti, Tanzania.

Suala linaloonyesha ongezeko dogo la ajira ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii katika nchi ya Tanzania, Profesa Winiesta Anderson kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema ongezeko dogo la ajira linatokana na uwezo mdogo wa wanafunzi wanaozalishwa katika vyuo vya utalii suala linalopelekea kuajiriwa kwa watoa huduma kutoka nchi za nje.

“kuna changamoto kwenye muktadha mzima wa ujuzi lakini pia sifa sahihi zinazohitajika katika sekta ya utalii kuhudumia watalii wakimataifa, ukienda visiwani unakuta kuna watoa huduma wengi kutoka nchi za nje kama Kenya, Italy na nyingine nyingi” ameongezea Anderson.

Siku ya Utalii Duniani 2024 ina kaulimbiu "Utalii na Amani," ikisisitiza jinsi utalii unavyoweza kuleta umoja, kuelewana, na amani kati ya jamii mbalimbali. Kaulimbiu hii inaonyesha umuhimu wa utalii kama daraja linalounganisha watu kutoka tamaduni tofauti na kuchangia katika uelewano wa kimataifa.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani sauti ya Amerika.

Forum

XS
SM
MD
LG