Miezi miwili na nusu imepita tangu wanamgambo wa Kiislamu waliposhambulia raia katika mji wa pwani wenye utajiri wa gesi wa Palma kaskazini mwa Msumbiji, na kuua darzeni ya watu na kuwakosesha makazi zaidi ya 70,000.
Huku viwango vya ghasia vikiwa vimepungua, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema mzozo wa silaha na ukosefu wa usalama unaendelea kuwakosesha makazi maelfu ya watu.
Msemaji wa UNHCR Babar Baloch anasema watu kila siku wanakimbia wakiwa wamekata tamaa kwa usalama kote nchini Msumbiji na upande mwingine wa mpaka nchini Tanzania.
“Watu 9,600 wamekata tamaa wakijaribu kutafuta hifadhi upande mwingine wa mpaka ndani ya Tanzania na kulazimishwa kurejea kwenye hatari kwa kweli tatizo na hali si nzuri…Wakimbizi wasirejeshwe walikotoka ambako kuna hatari,” Baloch anasema.
Anasema kwamba hiyo inakiuka misingi ya kutojazana au kurejeshwa kwa nguvu. Sheria ya kimataifa ya haki za binadamu inaeleza bayana kwamba hakuna mtu anatakiwa kurejeshwa katika nchi ambayo atakabiliwa na mateso au kutendewa mambo ambayo yanaweza kusababisha maumivu yasiyobadilika.
Baloch anasema timu za UNHCR kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji wanasema watu wanalazimishwa kurejea nchini Msumbiji wakati wamewasili wakiwa katika hali ya kukata tamaa. Anasema wengi wanatengana na familia zao na kuwaongezea madhila.
“Wale wanaorejeshwa kutoka Tanzania wanaishia kuishi katika mazingira mabaya sana mpaka wanakuwa katika hatari ya kukumbwa na manyanyaso ya kijinsia na hatari nyingine za kiafya kwa vile wanalala nje nyakati za usiku ambapo baridi ni kali sana hawana mablanketi au makazi ya muda kujisitiri. Kuna haja ya haraka kwa vifaa vya dharura vya misaada ikiwemo chakula kuwafikia,” Baloch anasema.
Mashirika ya kibinadamu yanakadiria takriban watu 800,000 wamekoseshwa makazi kaskazini mwa Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado tangu makundi yenye silaha, baadhi yana uhusiano na wanamgambo wa Islamic State, kuanzisha mashambulizi katika eneo hilo mwaka 2017.