Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:03

UNHCR yahofia mapigano Mashariki mwa DRC


Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC, likielekea katika mji wa Sakae kupambana na waasi wa M23. 09.02.2023. Picha na VOA
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC, likielekea katika mji wa Sakae kupambana na waasi wa M23. 09.02.2023. Picha na VOA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema Ijumaa kuwa "limepatwa na hofu kubwa" kutokana na mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo yamesababisha mamia ya watu kukimbia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh alisema ghasia hizo zimewafanya watu takriban 300,000 kuyahama maeneo yao huko Rutshuru na Masisi katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC mwezi Februari.

"Raia wanaendelea kulipa gharama kubwa kwa mgogoro huo unaosababisha umwagaji damu, wakiwemo wanawake na watoto ambao waliyakimbia maeneo yenye ghasia na sasa wanalala nje kwenye maeneo ya wazi, wakiwa wamechoka na wamekumbwa na kiwewe”, alisema msemaji wa UNHCR.

Saltmarsh pia alisema UNHCR na washirika wake wanazidisha misaada ya kibinaadamu, lakini bado ni vigumu kwa misaada hiyo kuwafikia watu waliopoteza makazi katika baadhi ya maeneo ya Kivu Kaskazini kwa sababu ya ghasia.

Katikati ya mwezi Januari, shirika la misaada la Umoja wa Mataifa OCHA lilisema, mashirika 12 yanayotoa misaada ya kibinadamu yalilazimika kusitisha shughuli zao katika sehemu za maeneo ya jimbo la Ituri kwa sababu ya ongezeko la mashambulizi.

Serikali ya Congo ilitangaza hali ya kuzingirwa kwa Kivu Kaskazini na eneo jirani la Ituri mwaka 2021 ikiwa ni jaribio la kuzuia kuenea kwa ghasia za wanamgambo katika eneo hilo la mashariki lenye utajiri mkubwa wa madini.

Mauaji na matukio ya waasi bado yanaendelea.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters

XS
SM
MD
LG