Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:23

Umoja wa Ulaya waongeza dola bilioni 3.5 kudhamini mfuko wa kufadhili msaada wa kijeshi wa Ukraine


FILE - Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba
FILE - Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba Jumatatu ameuhimiza Umoja wa Ulaya kuongeza msaada kwa Ukraine, wakati Umoja huo ukiwa tayari umeongeza dola bilioni 3.5 kudhamini mfuko unaotumika kufadhili msaada wa kijeshi wa Ukraine.

Kuleba aliuhutubia mkutano wa Baraza la Masuala ya Kigeni la EU kupitia video, na baadae kutuma ujumbe wa tweeter kuwa “anahimiza EU kuharakisha juhudi za kuishinda Russia kwa kuongeza misaada kwa Ukraine.”

Mkuu wa sera za kigeni wa EU Josep Borrell alisema hali ya Ukraine inabakia kuwa ni kipaumbele chao cha juu.

Josep Borrell
Josep Borrell

“Tutaendelea kuongeza maradufu msaada wetu wa kijeshi kwa kutoa vifaa na mafunzo,” Borrell aliandika kwenye ujumbe wa Tweet. “Kwa muda wote utakaohitajika.”

Makamu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar alisema Jumatatu kuwa majeshi ya Ukraine yalikuwa yamepata mafanikio kidogo upande wa mashariki wa nchi hiyo katika wiki iliyopita, na kuwa kuna mapigano makali yanayoendelea katika miji ya Lyman, Bakhmut, Avdiivka na Maryinka.

Maliar pia alisema kuwa wakati “hali upande wa kusini haijabadilika sana katika wiki iliyopita,” majeshi ya Ukraine kwa jumla yamekomboa kilomita za mraba 130 tangu kuanzisha mapambano kujibu mashambulizi mapema mwezi huu.

Jeshi la Ukraine lilisema Jumatatu majeshi yake yalitungua makombora ya masafa marefu matatu ambayo yalifyetuliwa na Russia kutoka Bahari ya Black Sea na pia ndege saba kati ya nane za Shahed zisizokuwa na rubani zilizotengenezwa Iran zinazotumiwa na Russia kushambulia.

Ndege zisizo kuwa na rubani zilizotengenezwa Iran
Ndege zisizo kuwa na rubani zilizotengenezwa Iran

Mashambulizi hayo ya angani yamekuwa ya kawaida katika uvamizi wa Russia huko Ukraine, huku maafisa wa Ukraine wakipongeza kazi ya mfumo wa ulinzi wa anga katika kuzuia mashambulizi hayo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema katika hotuba yake ya usiku Jumapili baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Joe Biden kuwa yeye “hasa anaishukuru” Marekani kutokana na mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot ulivyokuwa unajitosheleza.

Biden alisisitiza kuendelea kwa msaada wa Marekani kwa Ukraine ikiwemo kupitia msaada wa kiusalama, uchumi na kibinadamu, kulingana na taarifa ya White House.

Baadhi ya taarifa hii katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG