Katika maeneo mbalimbali nchini humo, ghasia zimeendelea kujitokeza huku Wakenya wengi wakionekana kujitenga na mchakato mzima. Watu wengi wameendelea kujiuliza ni kwa sababu gani hili linaendelea kutokea.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA amerepoti kuwa vyama vikuu kinzani vya kisiasa hususan Orange Democratic Movement kinachoongozwa na Raila Odinga pamoja na chama cha Jubilee ambacho kinapania kumhakikishia Rais Uhuru Kenyatta awamu ya pili madarakani, vimeonekana kukumbwa na ghasia za mara kwa mara; wawaniaji wakielezea kuhujumiwa katika mchakato mzima.
Wachambuzi wa kisiasa wamesema kuwa hata kama vyama hivi vikionekana kutokomaa kuandaa chaguzi za vyama, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakubaliana kuwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini unaonekana kuwafaidisha wanasiasa wachache wenye ushawishi mkubwa katika jamii zao na kuwapa madaraka makubwa katika umiliki wa vyama hivyo.
Sam Kamau mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Agakhan nchini anaeleza kuwa demokrasia katika vyama vya kisiasa nchini si komavu.
Aidha Kamau anashikilia kuwa bado hamna mafanikio makubwa ya vyama vingi nchini na kile kinachoshuhudiwa ni biashara za watu binafsi.
Na huku ikiwa dhahiri kuwa uwazi na usisitizaji wa demokrasia kwenye vyama vya siasa bado ni ndoto, Wakenya wengi wanaofuatilia siasa za vyama wanataraji pawe na heshima ya kidemokrasia kama njia mojawapo ya kufanya maamuzi yanayoafiki jamii pana.
Dunstan Omar, wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini anaeleza kuwa kutokana na rabsha na ukiukwaji wa haki na uwazi katika mchujo wa vyama, huenda pakawa na tatizo la maamuzi katika bunge lijalo pale patakapokuwa na wabunge wasioegemea vyama vyovyote. lakini pia amesema hali hii huenda ikaondoa kidonda cha ukabila.
Imeandikwa na Kennedy Wandera, Nairobi