Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 16:49

Polisi yachunguza uvunjifu wa amani Dar es Salaam


Simon Sirro
Simon Sirro

Watu watatu wanashikiliwa na polisi kufuatia tukio la uvunjifu wa amani katka mkutano wa kisiasa Dar es Salaam nchini Tanzania.

Washukiwa hao wamekamatwa kuhusiana na tukio la uvamizi katika mkutano wa mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kinondoni siku ya Jumamosi ya wiki iliyopita.

Katika mkutano wake na waandishi jijini Dar es Salaam Jumatatu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema shauri la kesi hiyo tayari limeshafunguliwa na upelelezi unaendelea.

Amesema uchunguzi huo unafanyika ili kuwabaini wale wote waliohusika na uvunjifu wa amani, huku akiwanasihi baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotoa vitisho kuwa watawafuata watu fulani kuwashughulikia.

“Hakuna mtu au kikundi cha watu wanaweza kuwa na mamlaka ya kuwashambulia wenzao… kama kuna malalamiko yapelekwe mahakamani,” amesema Sirro.

Kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa

Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi amelaani uvunjifu wa amani uliotokea wiki iliyopita katika hoteli ya Vina, Mabibo Dar es Salaam.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Jumatatu Jaji Mtungi amesema: “Ni ukweli usiopingika kuwa suala la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambulika na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF kutambua kwamba kuwapo kwa shauri mahakamani sio fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.”

“Ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa sheria.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hich au kujichukulia sheria mkononi.

XS
SM
MD
LG