Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:56

WHO yatangaza programu ya chanjo ya malaria Afrika


Ramani ya mafanikio ya kutokomeza ugonjwa wa malaria duniani (2010-2015).
Ramani ya mafanikio ya kutokomeza ugonjwa wa malaria duniani (2010-2015).

Shirika la Afya Duniani (WHO) limezichagua Ghana, Kenya na Malawi ambapo jaribio la chanjo ya malaria ya kwanza duniani litafanyika katika nchi hizo mwaka ujao kwa kuwahusisha watoto wadogo.

Habari hizi zimetangazwa na WHO wakati Jumanne dunia inasherekea siku ya malaria Duniani.

Dawa ya chanjo hiyo itayoingizwa mwilini mwao, inayojulikana kama RTS S au Mosquirix, imetengenezwa na Kampuni ya madawa ya Uingereza, GlaxoSmithKline.

Jaribio la chanjo hiyo litahusisha watoto wadogo wenye umri kati ya miezi 5 hadi 17.

Malaria ni ugonjwa ambao unahatarisha maisha unaosababishwa na vijidudu vinavyoenezwa kwa binadamu kupitia kungatwa na mbu wa kike mwenye ugonjwa huo.

WHO imesema katika tamko lake la programu hiyo ya majaribio “ itafanya tathmini ya uwezekano wa kuwapatia dozi zote nne zinazohitajika katika jaribio hilo ambapo zinawezesha kupunguza vifo vya watoto wadogo, na kuangalia usalama wake katika matumizi.

Mtizamo mzima wa chanjo ya malaria ni bishara nzuri. Taarifa zilizokusanywa katika majaribio zitaweza kutusaidia kufanya maamuzi juu ya uwezekano wa kutumia kwa upana zaidi chanjo hii,” amesema Dr Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Afrika.

“Pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na malaria, chanjo hii itakuwa na uwezo kuokoa maelfu ya maisha ya binadamu Afrika.

Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kuweka dawa kwenye chandarua na kunyunyizia dawa za kuua vijidudu hivyo ndani ya nyumba katika kuta zake.

Mnamo mwaka 2015, takriban watu 429,000 wamekufa kutokana na malaria, wengi wao ni watoto wadogo huko Afrika.

Juhudi za kimataifa zimeendelea kati ya mwaka 2000 na 2015, na hivyo kupelekea kupungua kwa vifo vinavyotokana na malaria kwa asilimia 62.

Kwa mujibu wa WHO, “Afrika inabeba mzigo mkubwa zaidi wa tatizo la malaria ulimwenguni.” Katika mwaka 2015, nchi zilizoko chini ya jangwa la Sahara lilikumbwa na asilimia 90 ya tatizo la malaria na asilimia 92 ya vifo inayotokana na ugonjwa huo.

XS
SM
MD
LG