Nyumba zaidi ya 150, mifugo, na mimea vimefunikwa na matope huku shughulii za uokoaji zikiwa zinaendelea.
Vijiji viwili vya Bunamwana na Bukobero, katika kata ndogo ya Buwali, wilayani Bududa, kwa mara nyingine ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, vinaomboleza tena kufuatia maporomoko ya matope, usiku wa kuamkia leo na kusababisaha hali ya majonzi wilayani humo.
Watu walikuwa wamelala
Msemaji wa shirika la msalaba mwekundiu Irene Nakasiita, kwenye ujumbe wa Twitter, ameandika kwamba maafisa wanaendelea na shughuli za uokoaji lakini hadi wakati tunaandaa ripoti hii, hakuna taarifa zaidi zilizotolewa juu ya kiwango cha uharibifu huo.
Lakini Nabende Wamoto, mkaazi wa eneo hilo anasema uharibifu huo ni mkubwa
“hali ni mbaya, usafiri umeharibika na kwa sasa watu wenyewe wanafanya juhudi za uokoaji. Tunatarajia maafisa wa jeshi kusalia kama ilivyo kawaida maporomoko yanapotokea. Hali ni ya majonzi”, amesema Wamoto
Tukio la leo linajiri mwaka mmoja baada ya mto Suume kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa na kusababisha maporomoko makubwa ya matope yaliyopelekea vifo vya watu 40.
Bududa inayopatikana karibu na mlima Elgon, kilomita 260 kutoka Kampala, mashariki mwa Uganda imekuwa sehemu hatari kwa makao ya watu kila msimu wa mvua, ikirekodi maporomoko ya matope kila mwaka.
Juhudi za serikali kuwahamisha watu kutoka sehemu zenye athari ya kutokea maporomoko ya matope hadi sehemu salama zimekosa kufaulu kutokana na ukosefu wa pesa.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Sauti ya Amerika, Washington DC