Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:47

Ufaransa yalaani mapinduzi ya kijeshi Gabon, UN na US wasisitiza utawala wa kidemokrasia


Rais wa Gabon aliyepinduliwa Ali Bongo Ondimba
Rais wa Gabon aliyepinduliwa Ali Bongo Ondimba

Ufaransa imesema Jumatano kuwa inalaani mapinduzi ya kijeshi  nchini Gabon na kurejea msimamo wake  kuwa lazima uwepo uchaguzi huru na wa wazi.

“Tunalaani mapinduzi hayo ya kijeshi na tunaelezea tena nia yetu ya dhati ya kuwepo uchaguzi huru na wa wazi,”, msemaji wa serikali ya Ufaransa Olivier Veran ameeleza.

Olivier Veran
Olivier Veran

Mapinduzi yanasababisha hali ya wasiwasi zaidi uwepo wa Ufaransa katika eneo hilo. Ufaransa ina wanajeshi 350 nchini Gabon. Majeshi yake yamefukuzwa Mali na Burkina Faso baada ya mapinduzi ya huko miaka miwili iliyopita.

Marekani

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby anasema kuwa:

“Hili tukio jeshi kuchukua madaraka, bila shaka la hivi karibuni katika kanda ambayo imekumbwa na mapinduzi ya kijeshi na unyakuzi wa madaraka kwa mabavu kinyume cha katiba. Na, hili tena, linatupa wasiwasi sana.

John Kirby
John Kirby

Tutaendelea kuwaunga mkono wananchi katika kanda hiyo na kuwasaidia watu wa Gabon na madai yao ya utawala wa kidemokrasia, bila shaka, lakini tutasema kuwa tunaendelea na lengo letu la kuendelea kufanya kazi na washirika wetu wa Afrika na, watu wote wa bara hilo kutatua changamoto mbalimbali na kusaidia demokrasia.”

“Tutaendelea na lengo letu la kuendeleza demokrasia katika bara hilo na duniani kote kwa sababu tunafikiria kuwa njia bora zaidi ya utawala bora ni kuendeleza amani na mafanikio ya wananchi.”

“Tutaendelea kufanya kila tunaloweza kuunga mkono maadili, maadili ya kidemokrasia, ambayo yanaonyeshwa na Waafrika katika bara lote.

Umoja wa Mataifa

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Thomas-Greenfield anasema kuwa:

Bado tunatathmini hali ilivyo, hivi inaendelea kujitokeza hivi sasa. Hatuna maelezo kamili, lakini tunaendelea kushauriana na wanachama wengine wa Baraza la Usalama kuhusu hatua gani tunaweza kuchukua.

Kama unavyojua wakati mapinduzi ya Niger yalipotokea, Baraza hili lilikutana kwa dharura na tulitoa tamko lenye msimamo thabiti.

Lakini tunaendelea na uchunguzi. Mpaka tufahamu kinacho endelea nchini humo, hatuwezi kuchukua hatua yoyote bado. Lakini nataka nieleze wazi, tunalaani hatua zozote za majeshi kunyakua madaraka kwa nguvu.

China

China imetoa wito kuwepo suluhisho la amani wakati Russia ikieleza inatarajia kutarejea utulivu wa haraka nchini Gabon.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin "China inafuatilia kwa karibu maendeleo ya hali nchini Gabon na kutoa wito kwa pande husika nchini Gabon kuzingatia maslahi ya msingi ya nchi na watu, kusuluhisha tofauti zilizopo kwa amani kupitia mazungumzo, na kurejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. Na pia kuhakikisha usalama wa Rais Bongo binafsi, kudumisha amani ya taifa, utulivu, na maendeleo ya ujumla."

Wang Wenbin
Wang Wenbin

Russia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia Maria Zakharova amesema Jumatano ana wasiwasi kuhusu hali iliyoko nchini Gabon kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na maafisa wa nchi hiyo.

Maria Zakharova
Maria Zakharova

"Moscow imepokea kwa wasiwasi ripoti za kuzorota kwa kiwango kikubwa cha hali ya ndani katika nchi hiyo ya kirafiki ya Kiafrika. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya hali hiyo na tunatumaini kuwepo kwa utulivu wa haraka", Waziri wa Mambo ya Nje Maria Zakharova aliwaambia waandishi wa habari.

Maoni ya Wananchi

Mamia ya watu wamesherehekea jeshi kuingilia kati, wakati Ufaransa, ambayo ni mtawala wa kikoloni wa zamani wa Gabon ambao wana wanajeshi nchini humo, wamelaani mapinduzi hayo.

“Ninaandamana leo kwa sababu ya furaha. Baada ya takriban miaka 60, utawala wa familia ya Bongo hauko madarakani,” alisema Jules Lebigui, kijana wa miaka 27 asiyekuwa na kazi ambaye aliungana na kundi kubwa katika mitaa ya Libreville.

Kamati ya Mpito

Maafisa hao wa jeshi la Gabon, wanaojiita Kamati ya Mpito na Kuziimarisha Taasisi, wakisema nchi hiyo inakabiliwa “na mgogoro mkubwa wa kitaasisi, kisiasa, kiuchumi na kijamii”. Wanasema uchaguzi wa Agosti 26 haukuwa halali.

Hata hivyo haikuwekwa bayana nani alikuwa anaongoza mapinduzi, lakini picha za televisheni zilikuwa zinamuonyesha mtu akiwa katika magwanda ya jeshi na kofia ya kijani wakipiga makelele “Oligui rais”, ikiashiria zaidi kuwa ni Brice Oligui Nguema, mkuu wa kikosi cha Gabon cha Republikan Guard.

“kufuatia viongozi hao wa mapinduzi kudai kuwa wanawakilisha vyombo vyote ya usalama ya Gabon, Bw Bongo hatarajiwi kuwa na uwezo wa kuzima mapinduzi hayo,” ameandika Rukmini Sanyal, mchambuzi katika Economist Intelligence Unit, akielezea “kuenea kwa kero la umma” dhidi ya Bongo, familia yake na chama chake tawala.

Kikundi cha maafisa wa jeshi katika nchi ya Afrika ya Kati ya Gabon wanasema wamemuondoa madarakani Rais Ali Bongo na kumweka katika kizuizi cha nyumbani.

Maafisa hao walitangaza mapinduzi yao mapema Jumatano asubuhi katika televisheni ya taifa Gabon 24, muda mfupi baada ya tume ya taifa ya uchaguzi ya taifa kutangaza kuwa Bongo alikuwa ameshinda muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi.

Maafisa hao walisema kuwa matokeo ya uchaguzi yamefutwa, na taasisi zote za serikali zimevunjwa na mipaka yote imefungwa hadi itakapotolewa taarifa zaidi.

“Tumeamua kulinda amani kwa kusitisha utawala wa hivi sasa,” mmoja wa maafisa hao wa jeshi alisema.

Licha ya kuwepo milio ya risasi kwa muda mfupi katika mji huo mkuu mara baada ya maafisa hao kutoa tangazo lao la kwanza, mitaa ya Libreville ilikuwa shwari mpaka pale tafrija zilipoanza. Maafisa wa polisi walipelekwa kulinda maeneo makuu ya jiji.

Bongo alichukua madaraka mwaka 2009, baada ya kifo cha baba yake, Omar Bongo ambaye alikuwa rais katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta tangu mwaka 1967.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii inatokana na mashirika ya habari ya Reuters, Agence France-Presse.

Forum

XS
SM
MD
LG