Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa viongozi wa Ulaya nchini Uingereza, Zelenskyy alisema anafikiri Marekani pia itakuwa tayari kutia saini mkataba huo wa madini, lakini inaweza "kuhitaji muda zaidi wa kutathmini baadhi ya mambo.
"Pande hizo mbili zilitarajiwa kutia saini makubaliano hayo wiki iliyopita wakati wa ziara ya Zelenskyy katika Ikulu ya Marekani, lakini mpango huo ulisambaratika baada ya majibizano makali ya maneno wakati wa mkutano na Trump na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance.
Zelenskyy amesema kwamba Ukraine inategemea msaada wa Marekani katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa miaka mitatu wa Russia
"Nadhani kusitisha msaada kama huo kutasaidia tu Rais wa Russia Vladimir Putin," Zelenskyy alisema. "Na kwa sababu hiyo, nadhani Marekani na wawakilishi wa ulimwengu uliostaarabika, viongozi wa dunia hii, hakika hawatamsaidia Putin."
Trump alimtaja Zelenskyy kama asiye na shukrani wakati wa mkutano wao wa Ijumaa na anataka kutumia mpango huo wa madini kama njia ya kufidia Marekani kwa mabilioni ya dola za msaada, ambayo imetoa kwa Ukraine.
Wakati huo huo, KremlinJumatatu ilimshutumu Rais Volodymyr Zelensky kwa kutotaka amani, kufuatia makabiliano ya wiki iliyopita kati ya kiongozi huyo wa Ukraine na Rais wa Marekani Donald Trump.
"Hataki amani. Mtu anapaswa kumlazimisha atafute amani. Ikiwa ulaya itafanya hivyo, heshima zote kwao," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari.
Alielezea mkutano uliokwa na majibizano Ijumaa kati ya Trump na Zelensky kama "tukio ambalo halijawahi kutokea".
Alielekeza lawama kwa Zelensky, ambaye alisema "alionyesha ukosefu kamili wa uwezo wa kidiplomasia.”
Peskov alisema Rais Vladimir Putin alikuwa anafahamu kilichotokea, akisema tukio hilo lilithibitisha mtazamo wa Russia kuhusu mzozo huo kuwa sahihi. Alisema washirika wa Ulaya pia watalazimika kumtuliza Trump, akisema "mtu atalazimika kufanya juhudi kubwa katika mazungumzo na Washington ili kwa njia fulani kufuta hali isiyopendeza katika White House baada ya kuzungumza na Zelensky".
Katika hali hii, "ni wazi juhudi za Washington pekee na utayari wa Moscow hautatosha," Peskov alisema.
Kremlin ilitoa maoni yake baada ya washirika wa Ukraine wa Ulaya kufanya mazungumzo ya dharura mjini London mwishoni mwa juma, huku Zelensky akisema atafanya kazi na Ulaya kuweka masharti ya makubaliano ya amani yanayoweza kufanyika.
Forum