Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:08

Tanzania yatangaza siku nne za maombolezo


Shughuli za uokoaji zikiendelea katika ajali ya Ferry MV Nyerere katika ufukwe wa kisiwa cha Ukerewe, ziwa Victoria, Tanzania, Septemba 21, 2018
Shughuli za uokoaji zikiendelea katika ajali ya Ferry MV Nyerere katika ufukwe wa kisiwa cha Ukerewe, ziwa Victoria, Tanzania, Septemba 21, 2018

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ametangaza siku 4 za maombolezo kuanzia Ijumaa kufuatia ajali ya Ferri ya MV Nyerere iliyozama katika ziwa Victoria siku ya Alhamisi.

Katika ajali hiyo, watu zaidi ya 130 wamethibitishwa kupoteza maisha kufikia Ijumaa, huku wengine zaidi ya 40 wakiwa tayari wamesha okolewa. Serikali imesema zoezi hilo la uokoaji linaendelea.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba mizigo na abiria wengi zaidi ya uwezo wake. Serikali tayari imetuma wachunguzi katika eneo la tukio la ajali hiyo kufanya uchunguzi wa kina.

Rais Magufuli ameagiza watendaji wa Kivuko na wengine wote wakamatwe katika hali ya uchunguzi huo, akiwemo kapteni wa meli hiyo.

Shirika la habari la Reuters liliwanukuu maafisa wa serikali ya Tanzania wakisema kuwa wanahofia huenda watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Maafisa wa usafiri wanasema Ferry ya MV Nyerere inauwezo wa kuchukua abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda waliohojiwa na vyombo vya habari vya Tanzania walisema kwamba wakati wa ajali hiyo, feri hiyo ilikuwa imebeba watu wengi kupita kiasi.

Ijumaa usiku, maafisa wa serikali ya Tanzania walisema huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.

Feri hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa watu wa Ukerewe tangu 2004.

XS
SM
MD
LG