Partika Munyu mfugaji kutoka wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani anasema wamekuwa wakipitia changamoto nyingi kama vile migogoro ya ardhi na wakulima, ukosefu wa maji na elimu kwa watoto kutokana na kuhama mara kwa mara pamoja na magonjwa kwa mifugo kwa sababu ya ukosefu wa wataalamu.
Munyu anasema: Huko nyuma tulikuwa tunakumbana na changamoto ya migogoro ya ardhi ya mara kwa mara baina yetu na wakulima, mifugo inakuwa ni dhaifu kwa sababu ile hali ya kuhama hama mara kwa mara ina changamoto za kupatikana maji.
Wafugaji hao wameendelea kusema uwepo wa miundombinu bora ndio silaha kwa mfugaji na itawasaidia kupambana na magonjwa ya mifugo pamoja na kuhama kutoka kwenye ufugaji wa kitamaduni kuelekea kwenye njia za kisasa.
Solomoni Olomoge mmoja ya wafugaji hao anasema serikali iendelee kutoa elimu kwa wafugaji pamoja na kutengeneza miundombinu ikiwemo majosho ya kuoshea ng’ombe.
Olomoge amesema:“Lakini pia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambao ndio mkombozi kwa mfugaji ili uweze kupambana na magonjwa lazima uwe na miundombinu mizuri ikiwemo kama majosho ni vitu ambavyo vinamuwezesha mfugaji kupambana na magonjwa nyemelezi na yanayoleta uharibifu kwa mifugo.
Kwa muda mrefu tatizo la jamii ya kimasai limekuwa ni maeneo ya malisho, Emanuel Olenasha mfugaji kutoka Mkuranga ameitaka serikali kuwatengea maeneo maalumu kwaajili ya kufanya ufugaji kwa njia ya vitalu kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya wilaya.
Olenasha anasema: “Wafugaji wengi wa Tanzania hasa jamii ya Wamaasai na Wasukuma mpaka Wamang’ati; wafugaji ambao ni wafugaji wa kuhamahama kufuata malisho na maji kunachangamoto sana kwasababu hawajatengewa maeneo ya kutosha wakawa wanafuga kwa vitalu.’’
Waziri wa mifugo na uvuvi wa Tanzania Abdallah Ulega amesema serikali imeandaa mpango wa jenga kesho bora kwa upande wa mifugo ambao unalenga kuwaandaa wafanyabiashara na siyo watu wa kuchunga sambamba na utoaji wa elimu na kuwamilikisha ardhi.
Ulega anaeleza: Tunahamasisha sana wamiliki ardhi badala ya kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kila mara wanahama ambayo katika hatua hizo za kuhama zinaacha ugomvi mkubwa na kusababisha mitafaruku katika jamii. Kwa hiyo hizi hatua pamoja na hatua nyingine ndizo tunaziwekea mkazo zaidi.
Wafugaji wanasema ili miradi kama hii iweze kuendelea basi ina wajibu wa kuwaunga mkono hususani kuwapatia maeneo kwa ajili ya malisho.
Amri Ramadhani, VOA, Pwani, Tanzania.
Forum