Kulingana na wanafamilia Waziri alifariki baada ya kuugua ghafla na kuharakishwa katika hospitali ya Mwananyamala mjini Dar es salaam. Chanzo kamili cha kifo chake hakijaelezwa.
Waziri alikuwa kiongozi wa bendi ya Kilimanjaro kwa miaka mingi akishirikiana na wanamuziki wengine mashuhuru kama vile marehemu Mabruk “Babu Njenje” Hamisi, Mohamed Mrisho, Nyota Waziri, Keppy, John Kitime na wengineo
Waziri alianza kupiga muziki akiwa mdogo sana na bendi za muziki wa taarab mjini Tanga kama vile Lucky Star na Black Star. Uhodari wake wa kupiga kinanda ulimpa umaarufu hadi kuajiriwa na bendi za muziki wa dansi kama Nuta Jazz ya mjini Dar es salaam
Baadaye Waziri alijiunga na bendi ya vijana wenzake kutoka mjini Tanga, Kilimanjaro Band katika miaka ya 80 na kuanzia hapo hakutoka katika bendi hiyo hadi alipochukua uongozi wake katika miaka 90 baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo Hemed Chuky.
Waziri aliiongoza bendi ya Kilimanjaro katika mikataba mingi ya kimataifa iliyowawezesha kupiga muziki katika nchi za Japan, Uingereza na nchi Falme za Kiarabu.
Baada ya kutoa album ya Njenje, ambayo ilifanya bendi hiyo kujulikana kwa jina la Njenje – Kilimanjaro Band ilitoa album nyingine kadha zikiwa na nyimbo ziligonga chati kama vile Boko, Kinyaunyau, Kachiri, Tupendane, Ndembele, na Ndugu Zangu.