Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 26, 2024 Local time: 18:22

Sheria ya Ushoga Uganda ifutwe haraka - Biden


Rais wa Marekani Joe Biden, akiwa na Makamu wa Rais Kamala Harris (kushoto) huko Washington, DC, tarehe 25 Mei 2023. Picha na Mandel NGAN/AFP.
Rais wa Marekani Joe Biden, akiwa na Makamu wa Rais Kamala Harris (kushoto) huko Washington, DC, tarehe 25 Mei 2023. Picha na Mandel NGAN/AFP.

Rais wa Marekani Joe Biden Jumatatu ameishutumu sheria mpya ya Uganda inayopinga mapenzi ya jinsia moja na kusema kuwa inakiuka haki za binadamu, na inahatarisha maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo iliyoko mashariki mwa bara la Afrika.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa siku ya Jumatatu, Rais Biden alilaani hatua hiyo ya kupitishwa kwa mswaada huo wa sheria wenye utata unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja, ikiwa pamoja na adhabu ya hadi miaka 10 jela na faini ya hadi shilingi milioni 10 za Uganda.

Sheria hiyo pia inatoa adhabu ya kifo kwa "ushoga uliokithiri," kosa ambalo ni pamoja na kusambaza UKIMWI kupitia ngono ya mashoga.

Rais Biden alisema “Ninaungana na watu duniani kote wakiwemo watu wengi wa Uganda katika kuitaka sheria hiyo ifutwe mara moja” na kuongeza kuwa, “hakuna mtu anayestahili kuishi kwa kuhofia maisha yake wakati wote au kufanyiwa vitendo vya ukatili na ubaguzi. Ni makosa”

Rais Museveni aliupitisha mswaada huo wenye adhabu kali dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kuwa sheria ya ushoga ya mwaka 2023 siku ya Jumatatu, baada ya kufanyiwa marekebisho ambayo vipengele vingi vyenye msimamo mkali havikurekebishwa.

Taarifa iliyochapishwa kupitia akaunti rasmi ya Twitter ya Rais huyo wa Uganda imeeleza kuwa Museveni ameukubali mswaada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja wa mwaka 2023, Sasa unakuwa Sheria ya kupambana na mapenzi ya jinsia moja 2023.

Pia bunge la Uganda kupitia ukurasa wake wa Twitter limesema wabunge wamechukua hatua hiyo ili kulinda utamaduni na maadili ya taifa hilo.

Mwezi machi mwaka huu, rais huyo aliyekuwa madarakani kwa takriban miongo minne aliwaelezea mashoga kuwa ni "wapotovu" na "ni mwenendo wa tabia unaokiuka maadili".

Mswaada huo ambao umekuwa sheria pia unawagusa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wamiliki wa nyumba na hoteli, wamiliki wa vyumba vya burudani, waandishi wa habari, watengenezaji filamu na wengineo.

Adhabu kwa wanaoeneza habari za ushoga kwa kuchapisha vitabu pamoja na wafadhili watatozwa faini ya shilingi milioni 100 za Uganda. Wanaomiliki vyumba vya kufanyia ushoga watahukumiwa miaka 7 jela wakati wamiliki wa nyumba watakaokodisha kwa mashoga watahukumiwa mwaka mmoja gerezani.

Tangu mswaada huo ulipofikishwa bungeni, watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wamekuwa wakikamatwa, kufukuzwa na wenye nyumba za kupanga na matukio mengi ya vitisho, unyanyasaji, ghasia na ubaguzi dhidi yao.

MARIAM MNIGA, SAUTI YA AMERIKA, WASHINGTON DC.

Forum

XS
SM
MD
LG