Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 09:51

Serikali yaunda tume ya watu 14 kupitia changamoto zilizoorodheshwa na wafanyabiashara


Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamebeba mabango kueleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa. Picha na Amri Ramadhani.
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamebeba mabango kueleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa. Picha na Amri Ramadhani.

Serikali ya Tanzania imeunda tume ya watu 14 kati ya hao saba kutoka kwa wafanyabiashara na saba kutoka serikalini kwa lengo la kupitia changamoto zote zilizo orodheshwa na wafanyabiashara hao.

Wafanyabiashara wamemueleza Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kuwa vitendo vya rushwa vinavyoendekezwa na Mamlaka ya Mapato nchini pamoja na Jeshi la Polisi vinapelekea kuwakimbiza wafanyabiashara wengi kuikimbia nchi hiyo kibiashara.

Wakati mgomo wa kufunga biashara katika soko la kimataifa la Kariakoo kushika kasi kwa siku ya tatu sasa, baadhi ya wafanyabiashara hao wamemueleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika kuwasikiliza Jumatano kuwa viongozi wengi wenye nafasi Serikalini hawapo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kujikwamua kiuchumi.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyefahamika kwa jina la Aziza Othumani amesema tabia ya ukamataji holela inayofanywa na Mamlaka ya Mapato kwa watu wanaoitwa Vishoka inawaumiza wafanyabiashara hali inayopelekea kuwadidimiza kiuchumi na kushindwa kufikia malengo yao.

Aziza anaeleza: "Kawaida biashara inatakiwa ikue lakini mnavyotufanyia mnatudidimiza watu wa TRA na mapato tunashindwa kukua kiuchumi."

Mfanyabiashara Juma Rashidi akizungumza kwa uchungu amesema utaratibu unaotumiwa na mamlaka ya mapato si rafiki kwao.

Amesema hatua hiyo inayopelekea kuwafukuza wafanyabiashara wengi huku akiongeza kuwa baadhi ya viongozi wa mamlaka hiyo hawapo kwa ajili ya Serikali bali ni kwa ajili ya matumbo yao.

Rashidi ameeleza kuwa: "Yaani wakiona tu mzigo umekuja ni wawachina huu ndio TRA hapo hapo wanakuna matumbo maana wanajua huu mzigo huu wa Wachina lazima tule tu."

Wakati huo huo Waziri Mkuu mara baada ya kusikiliza hoja za wafanyabiashara hao ameamua kuunda tume ya watu 14 ambapo 7 kutoka Serikalini na 7 wengine kutoka upande wa wafanyabiashara ili kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara na kero zao.

Majaliwa amesema: " Kwa ombi lililotolewa hapa na wazungumzaji kadhaa kwamba nilazima tuwe na tume ya pamoja ili ikae ikumbushane yale ambayo hayakujibiwa leo lakini yaingie yafanyiwe maboresho.

Baada ya kauli hiyo ya waziri mkuu wafanyabiashara wamekubaliana siku ya kesho kuendelea na shughuli zao katika soko la Kariakoo na kuisisitiza serikali kuzifanyia marekebisho sheria zote kandamizi kabla ya bunge la katiba kumaliza muda wake.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam.

XS
SM
MD
LG