Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:55

UN : Sababu zinazozuia uwepo wa familia ndogo nchi zinazoendelea


Ripoti ya mwaka 2018 ya Umoja wa Mataifa (UN) juu ya hali ya wakazi duniani inaonyesha kuwa kuna utamaduni wa watu kuwa na familia ndogo, lakini katika nchi zinazoendelea hilo bado ni changamoto.

Ripoti inaeleza kwamba ukubwa wa familia unakwenda sambasamba na haki ya uzazi na uwezo wa kuchagua idadi ya watoto mtu anaotaka kuwa nao.

Tamko la Monica Ferro

Mkurugenzi wa idara ya idadi ya wakazi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Monica Ferro anasema katika nchi ambazo haki za uzazi zinabanwa kutokana na ukosefu wa rasilmali au kanuni za serikali, hivyo watu hawana uwezo mkubwa wa kuchagua ukiubwa wa familia zao.

Wengi katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mfano anasema wana viwango vya uzazi mara nne au zaidi kwa kila mwanamke.

Pia tafiti hiyo imegundua kwamba watu katika nchi zilizoendelea, wana viwango vya chini zaidi vya uzazi kuliko wale wa nchi zinazoendelea.

Hii ni kwa sababu kwa kawaida wanauwezo mkubwa wa kupata huduma za uzazi wa mipango, mitindo mipya ya kuzuia uzazi na elimu ya ngono kulingana na umri unaostahiki.

Asia mashariki, Ulaya

Na kwa upande wa pili wa dunia una baadhi ya nchi za Asia mashariki na Ulaya ambako kuna kiwango cha chini katika familia kwa mwanamke kuwa na watoto wawili. Hata hivyo katika kanda hizo mbili watu wanakabiliwa na vipingamizi vya kutekeleza kikamilifu haki zao za uzazi.

Idadi ya wakazi duniani inatarajiwa kuongezeka kwa bilioni 2 na nusu kufikia 2050, hivyo kuwepo na watu bilioni 10 duniani. Ferro anasema nchi za Afrika zinatarajiwa kuchangia zaidi ya nusu ya ukuwaji huo. Ameiambia Sauti ya Amerika kuwa wanawake barani Afrika wanalazimika kupambana na vizuizi vingi vya kisheria na kijamii ili kuweza kudhibiti haki ya uzazi.

Huduma za afya

Wanawake huenda hawana uwezo wa kupata huduma za afya, kwani hawapati huduma za kuwaacha watoto wao wanapohitaji kufanya kazi. Huenda hawapati msaada wa kijami au kitaasisi ili kuweza kuwa tayari au kuweza kupanga uzazi wao wenyewe.

Ripoti hiyo inahimiza mataifa kutoa huduma za afya kwa wote pamoja na huduma za uzazi ikiwa ni pamoja na njia mpya za uzazi wa mpango na kuhakikisha elimu bora zaidi inapatikana. Inasisitiza kuhamasisha mabadiliko katika tabia ya wanaume kuelekea haki za wanawake kuchagua idadi , wakati na mpangilio wa kupata watoto.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG