Msemaji wa White House Jay Carney amesema rais Obama alichukua uwamuzi wake wa kutotoa picha za mwili wa Osama bin Laden kwa sababu mbali mbali za usalama wa taifa.
Carney alisema rais alikuwa na wasi wasi kwamba kuchapisha hadharani picha hizo za kuchukiza kunaweza kuwa na hatari kwa usalama wa kitaifa.
Carney alisema rais akihojiwa na kituo cha televisheni ya CBS alisema kwamba hakuna shaka kuna miongoni mwa wanachama wa al Aaida wanaamini bin Laden amefariki. Msemaji wa white house alimnuku bw Obama akisema, “hautamuona Osama bin Laden akitembea tena kwenye dunia hii”.
Carney anasema kwamba rais anashikilia msimamo wake unaoungwa mkono na waziri wa ulinzi Robert Gates na waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton
Lakini mkurugenzi wa CIA Leon Panetta ambae Bw. Obama amemteua kuwa waziri wa ulinzi kuchukua nafasi ya Bw. Gates amesema hadharani mara kadhaa kabla ya uwamuzi kutolewa kwamba inabidi picha hizo zitolewe.
Mjadala unaojitokeza ni kwamba baadhi ya wachambuzi hapa Marekani wanasema ni lazima kuchapisha picha ili kunyamazisha tetesi kwamba ni uwongo Osama hakuuliwa.