Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 12:52

Maelezo yatolewa kuhusu operesheni iliyomwua Osama


Nyumba ambayo Osama bin Laden inaaminika alikuwa akiishi karibu miaka 5 huko Abbottaba hadi alipovamiwa na kuuawa, May 1, 2011.
Nyumba ambayo Osama bin Laden inaaminika alikuwa akiishi karibu miaka 5 huko Abbottaba hadi alipovamiwa na kuuawa, May 1, 2011.

Maafisa wanasema Bin Laden aliishi katika makazi hayo kwa miaka ipatayo mitano, ikiwa na ulinzi mkali pamoja na kuta nene na senyenge

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu baada ya Rais Obama kuhutubia taifa Jumapili usiku, maafisa wa ngazi za juu wa Marekani walitoa maelezo zaidi kuhusu operesheni iliyomwua bin Laden, ingawa walisisitiza kuwa hawatafichua maelezo ya ndani ya operesheni hiyo.

Maafisa walielezea kile walichoita operesheni ya hatari iliyotumia helikopta ndogo iliyobeba makomando wa Kimarekani kuvamia eneo la jumba alimokuwa akiishi bin Laden nje kidogo ya mji wa Abbottabad, kaskazini ya mji mkuu Islamabad.

Maafisa wanasema makazi hayo yalikuwepo kwa karibu miaka mitano, huku yakiwa na ulinzi mkali, kuta nene zilizowekwa senyenge juu, madirisha machache yanayotokeza nje na milango miwili ya ulinzi. Hakukuwa na simu wala huduma za internet ndani ya makazi hayo.

Ramani ya nyumba ambayo Osama Bin Laden alikuwa akiishi na kuuliwa huko Abbottabad, Pakistani. Picha ilitolewa na CIA.
Ramani ya nyumba ambayo Osama Bin Laden alikuwa akiishi na kuuliwa huko Abbottabad, Pakistani. Picha ilitolewa na CIA.

Bin Laden alipigana

Kulingana na maafisa wa Marekani bin Laden alipambana na vikosi vya uvamizi na aliuawa katika mapigano hayo. Maafisa wa Marekani hawakutoa maelezo zaidi ya muda gani mapigano hayo yalidumu.

Timu ya kikosi maalum cha Marekani ilitumia kiasi cha dakika 40 tu na hakikuwa na mawasiliano yoyote na maafisa wa Pakistan. Wanasema operesheni hiyo ilipangwa kupunguza uwezekano wa watu wasiodhamiriwa kudhurika.

Katika mapigano hayo, maafisa wanasema, wanaume watatu waliuawa ikiwa na watu wawili wanaodhaniwa wasaidizi wa Obama waliokuwa wakitumiwa kutoa na kuleta ujumbe katika makazi hayo, pamoja na mtoto mmoja mkubwa wa bin Laden.

Kati ya wanawake kadha na watoto katika jumba hilo, maafisa wanasema mwanamke mmoja aliuawa alipotumiwa kama ngao na mpiganaji mmoja mwanamume. Wanawake wengine wawili walijeruhiwa.

Marekani ilipoteza helikopta moja

Moja ya helikopta za Marekani iliteketea katika operesheni hiyo kutokana na tatizo la kiufundi, maafisa hawakutoa maelezo zaidi.Walisema tu kuwa ndege hiyo iliteketezwa na kikosi cha Marekani kwa sababu za kiusalama, na wanajeshi waliobaki walipanda helikopta ya pili na kuondoka katika eneo hilo.

Maziko ya bin Laden

Akijibu swali, mmoja wa maafisa wa Marekani alisema hatua zote zilichukuliwa kuhakikisha mwili wa bin Laden unazikwa "kulingana na kanuni za kiislamu" kitu ambacho alisema Marekani inakitilia maanani.

Bin Laden alizikwa baharini kutokana katika meli moja ya kivita ya Marekani.

XS
SM
MD
LG