Mwanafunzi huyo William Mayange alikuwa ni miongoni mwa waandamanaji wa chuo hicho waliovamia kituo cha polisi na kusababisha maafisa wa polisi kutumia risasi kuwatawanya.
Katika mapambano hayo, polisi walifyatua risasi ambayo ilimpiga shingoni mwanafunzi huyo na kufariki baada ya kufikishwa katika hospitali ya Coptic, Kisumu. Kulingana na taarifa ya Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya Japheth Koome.
Waandamanaji wengine waliingia katika barabara za mji mkuu wa Nairobi, na miji mingine kadhaa kuitikia wito kutoka kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Baadhi ya waandamanaji hao waliwasha moto mitaani na kuwarushia mawe polisi. Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kuwarushia maji yanayowasha waandamanaji hao ukiwemo msafara wa Odinga aliyekuwa akiwahutubia wafuasi wake kutoka kwenye paa la kwenye gari yake.
Polisi walisema maafisa 24 walijeruhiwa katika mapambano hayo. Lakini hawakutoa idadi ya waandamanaji waliojeruhiwa. "Mapambano hayo ya siku nzima yaliyoshuhudiwa jana huko Nairobi na kisumu hayakuwa na msingi zaidi ya kufanya ghasia dhidi ya polisi na kuhujumu uchumi,” walisema polisi katika taarifa ya Jumanne.
Wakati akiitisha maandamano, Odinga, mwenye umri wa miaka 78, alielezea bei za juu za vyakula vikuu kama vile a unga wa mahindi, ambao umesababisha mfumuko wa bei kuwa juu.
Odinga pia alimshutumu Ruto kwa udanganyifu wa kura wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana. Ikiwa ni mara ya tano mfululizo kwa Odinga kugombea nafasi urais nchini humo alikuwa mshindi wa pili. Odinga alipinga matokeo hayo katika mahakama ya juu ambayo iliidhinisha ushindi wa Ruto.
Jumanne Odinga aliongeza wito wake wa kutaka maandamano yafanyike mara mbili kwa wiki, na kuzitaja siku za Jumatatu na Alhamisi kuwa siku za maandamano kuanzia Machi 27.
Wabunge wanne walikuwa ni miongoni mwa waliokamatwa wakati wa maandamano, wakiwemo viongozi wa kundi la Odinga katika mabaraza yote mawili ya bunge.
Wabunge hao waliachiwa kwa dhamana na watafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi kujibu mashtaka ya mkusanyiko usio halali, wakili wao, Danstan Omari, aliliambia shirika la habari la Reuters.