Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 00:58

Wabunge wa chama tawala washinikiza polisi kuwakamata Raila na Kenyatta


Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga (kushoto) na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta
Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga (kushoto) na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta

Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi nchini Kenya (IPOA) Jumanne imesema kuwa inachunguza jinsi maafisa wa polisi walivyokabiliana na waandamanaji 238 Jumatatu nchini humo.

IPOA inasema maafisa hao wanakiri kumuua muandamanaji ambayo ni mwanafunzi wa chuo kikuu huko Kisumu wakati waandamanaji kadhaa walipovamia kituo cha polisi.

Hata hivyo Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome alisema polisi walifanya kazi yao kwa njia ya kitaalamu.

Katika maandamano hayo jana Polisi imesema iliwakamata watu 25.

Maandamano yaliyofanyika Eastleigh karibu na Nairobi, Kenya, Machi 20, 2023. REUTERS/Thomas Mukoya
Maandamano yaliyofanyika Eastleigh karibu na Nairobi, Kenya, Machi 20, 2023. REUTERS/Thomas Mukoya

Idadi ya Waandanamaji Waliokamatwa

IGP amesema jumla ya watu waliokamatwa na polisi hadi kufikia Jumanne imefikia 213.

Pia ameeleza maafisa 7 wa polisi walijeruhiwa huko Nyanza; wakati mjini Nairobi magari 10 ya polisi yaliharibiwa na polisi 24 walijeruhiwa.

Wakati huo huo wabunge wa serikali wanaendelea kuwashinikiza polisi kumkamata kiongozi wa upinzani Raila Odinga na rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa madai ya kufadhili maandamano hayo.

Mwanafunzi Afariki kwa Kupigwa Risasi

Taarifa ya mamlaka hiyo inafuatia ripoti za kupigwa risasi kwa William Mayange na kufariki, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno mjini Kisumu, Magharibi mwa Kenya.

Taarifa ya Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya Japheth Koome inaeleza kuwa waandamanaji ambao walijumuisha wanafunzi wa chuo hicho walivamia kituo cha polisi na kusababisha maafisa wa polisi kutumia risasi kuwatawanya, makabiliano yaliyosababisha mwanafunzi huyo kupigwa risasi shingoni na kutangazwa kufariki alipofikishwa katika hospitali ya Coptic, Kisumu.

Mamlaka hiyo ya kutathmini utendaji wa polisi, inaeleza kuwa imeanzisha uchunguzi wa tukio hilo na matukio mengine ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na polisi ili kuwawajibisha kisheria.

Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga akiongea na wafuasi wake katika mtaa wa Eastleigh jirani na Nairobi, Kenya, Machi 20, 2023.
Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga akiongea na wafuasi wake katika mtaa wa Eastleigh jirani na Nairobi, Kenya, Machi 20, 2023.

Maafisa wa Polisi Watekeleza Wajibu Wao

Hata hivyo, Koome, amevieleza vyombo vya habari kuwa maafisa wa polisi waliokabiliana na waandamanaji Jumatatu walitekeleza wajibu wao kwa utaalam wa juu na kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia haki za binadamu licha ya kila mara kulazimika kuvumilia vitendo vya waandamanaji waliojihusisha na matukio ya uhalifu wa vurugu pamoja na kuwarushia mawe maafisa wa polisi wa kutuliza ghasia.

Zaidi ya hayo, Bw Koome anaeleza kuwa huduma ya polisi iko tayari kuwajibikia vitendo vyao na ipo tayari kuchunguzwa na mashirika huru na ya kikatiba.

Lakini wakati vumbi la maandamano ya upinzani nchini Kenya likionekana kutulia huku wafanyabiashara wakiendelea kukadiria hasara iliyosababishwa na usitishwaji wa ufanyikaji wa biashara katika miji mikuu ya Kenya, Jumatatu, Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza kuwa maandamamano dhidi ya utawala wa rais William Ruto yajayo yatafanyika kila Jumatatu na Alhamisi.

Odinga Awataka Wafuasi wake Kususia Makampuni na Mashirika ya Habari

Aidha, Odinga anawataka wafuasi wake kususia makampuni ya benki na baadhi ya mashirika ya vyombo vya habari, kwa kile anachodai kuwa ni kuwa sehemu ya wawezeshaji wa utawala wa kikatili na maadau ya wa watu.

Na kuhusu mwenendo wa maafisa wa polisi, upinzani unasema kuwa umeanzisha uchunguzi kubaini maafisa wa polisi waliotumia nguvu kupita kiasi na kisha kuwafungulia mashtaka, kila mmoja.

Wabunge wa Chama Tawala

Awali, wabunge wanaoegemea upande wa serikali, wanamshinikiza Inspekta wa polisi Japheth Koome kumkamata Odinga na viongozi wengine wa muungano huo kwa kuongoza maandamano yaliosababisha uharibifu wa mali. Pia, wanataka rais mstaafu Uhuru Kenyatta kukamatwa kwa madai ya kufadhili maandamano ya upinzani, anavyoeleza Kiongozi wa shughuli za serikali katika bunge la Kitaifa, na mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung'wa.

Katika miji ya Kisumu, Mombasa, Migori, Homabay, Nakuru, Siaya, Kakamega, Kitale na jiji la Nairobi, polisi wa Kenya walilazimika kuwatawanya mamia ya waandamanaji wa upinzani kwa kurusha gesi za kutoza machozi na kutumia magari ya maji, walionuia kuishinikiza serikali kukabili ugumu wa ufikiaji wa gharama ya bidhaa za kimsingi na kumtaka rais kuondoka mamlakani wakidai kuwa hakuchaguliwa kwa njia halali.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi.


XS
SM
MD
LG