Mazungumzo kati ya Russia na Ukraine yameanza katika mpaka wa Belarus Jumatatu wakati ambapo Russia inazidi kutengwa kidiplomasia na kiuchumi siku nne tangu ilipoivamiaUkraine, ikiwa ni shambulizi kubwa kufanyika katika nchi ya Ulaya tangu vita vya pili vya dunia.
Vikosi vya Russia vimeteka miji miwili midogo kusini mashariki mwa Ukraine na eneo kuzunguka kiwanda cha nyuklia, shirika la habari la Intefax limeripoti leo, lakini walikumbana na upinzani mkali.
Mazungumzo yameanza kwa lengo la kusitisha mapigano na kuondoa wanajeshi wa Russia, ofisi ya rais wa Ukraine imesema.
Hata hivyo operesheni za Russia zimekwenda taratibu tofauti na wengine walivyotarajia.
Russia imekataa kutoa maelezo yoyote , na haiko bayana kama kuna maendeleo yoyote yanaweza kupatikana baada ya Rais Vladmir Putin Alhamisi kufanya shambulizi na kuweka kikosi cha nyuklia cha Russia katika hali ya tahadhari.
Mazungumzo yanafanyika katika mpaka na mshirika mkubwa wa Russia, Belarus ambapo kura ya maoni siku ya jumapili iliidhinisha katiba mpya inayoondoa hali ya kutokuwa na nyuklia ya nchi hiyo wakati ambapo jamhuri ya zamani ya Soviet imekuwa uwanja uliotumiwa na wanajeshi wa Russia walioivamia Ukraine.
Majibu ya nchi za magharibi kwa uvamizi huo yamekuwa makubwa wakiweka vikwazo ambavyo zimezuia taasisi kuu za kifedha za Moscow kutoka kwenye masoko ya hisa ya magharibi hatua ambayo imesababisha sarafu ya Russia kushuka kwa asilimia 30 dhidi ya Dola Jumatatu.
Baadhi ya nchi pia zimeongeza usambazaji wake wa silaha kwa Ukraine.