Rais Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kwa mzungumzo ya amani, bila ya masharti yoyote na Russia, kwenye mpaka wake na Belarus katika eneo maalum karibu na Chernobil, baada ya kuwa na mazungumzo na rais wa Belarus Alexander Lukashenko Jumapili.
Rais Zelensky anasema Belarus haiwezi kuwa mwenyeji wa mazungumzo kwa sababu Russia imetumia nchi hiyo kuanzisha uvamizi dhidi ya nchi yake.
Rais Vladimir Putin amesema kwamba tayari kuna ujumbe wa Russia katika mji wa Gomel nchini Belarus kwa ajili ya mazungumzo.
Habari hizo zimetolewa wakati wanajeshi wa Russia wamekuwa wakipambana na wanajeshi na raia wa Ukraine walioamua kuchukua silaha katika mitaa ya miji mbali mbali, katika siku ya nne tangu kuanza uvamizi wa Russia.
Jumapili vile vile wanajeshi wa Ukraine wameweza kuchukua tena udhibiti kamili wa mji wa Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa baada ya mapigano makali na wanajeshi wa Russia.
Mkuu wa jimbo Oleg Sinegubov amesema kwenye ujumbe wa Telegram kwamba, mji wa Kharkiv umekombolewa kabisa na wanajeshi wa Russia wana furushwa katika operesheni za mwisho mwisho.
Mapigano makali yanaripotiwa pia katika mji wa Donetsk ambao umekua ukishikiliwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Russia tangu 2014.
Mapigano yakiendelea shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema zaidi ya watu laki mbili wameshakimbia kutoka nchi hiyo wengi wao wakikimbilia Poland na kwamba karibu watu milioni 4 wanatazamiwa kukimbia mnamo siku chache zijazo.
Hata hivyo maafisa wa Ukraine wanasema kuna zaidi ya watu laki tatu elfu 68 waliokimbia tayari.