Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 00:57

Mazungumzo ya kumaliza mapigano Sudan kuanza tena Jeddah


Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na makamu wake wa zamani, kamanda wa vikosi vya Msaada ya Dharura (RSF) Mohamed Hamdan Daglo (kulia)
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na makamu wake wa zamani, kamanda wa vikosi vya Msaada ya Dharura (RSF) Mohamed Hamdan Daglo (kulia)

Mazungumzo kati ya pande zinazopigana nchini Sudan yataanza tena Alhamisi huko Jeddah, Saudi Arabia, yakilenga fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia wanaokabiliwa na hali ngumu, kulingana na maafisa wakuu wa Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani.

Marekani na Saudi Arabia zimeratibu usitishaji mapigano mara kadhaa kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Jeshi la Wanajeshi wa Msaada wa Dharura (RSF) katika mazungumzo ya Jeddah tangu mwezi Mei, lakini mapigano yameendelea huko Khartoum na maeneo mengine, huku kila upande ukimshutumu mwenzake kwa kukiuka sitisho la mapigano.

Marekani iliahirisha mazungumzo hayo tarehe 21 Juni.

Wakati huo huo, Jeshi la Sudan na vikosi vya kijeshi vya Msaada wa Dharura (RSF) vilisema vitarejea katika mazungumzo yaliyoitishwa na Marekani na Saudi Arabia mjini Jeddah siku ya Alhamisi, wakati vita vya miezi sita vikiwa vimeiathiri nchi hiyo na pande zote za vikosi hivyo.

Jeshi la Sudan lilisema Jumatano limekubali mwaliko na utatuma ujumbe wake mjini Jeddah katika bahari ya Sham nchini Saudi Arabia, kukamilisha mazungumzo na vikosi vya kijeshi vya Msaada wa Dharura (RSF).

Mazungumzo ya Jeddah yanalenga kusimamisha kwa muda mapigano, kama siyo kuyamaliza kabisa ambayo yalizuka mwezi Aprili kufuatia mzozo wa madaraka kati ya jeshi na RSF juu ya masharti kwa ajili ya mabadiliko ya taratibu kutoka utawala wa kijeshi kelekea demokrasia.

Kutoka kushoto ni Jenerali Mohamed Hamdan Daglo "Hemeti", akizungumza na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huko Khartoum tarehe 8 Oktoba 2020 Picha na Ebrahim HAMID / AFP.
Kutoka kushoto ni Jenerali Mohamed Hamdan Daglo "Hemeti", akizungumza na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huko Khartoum tarehe 8 Oktoba 2020 Picha na Ebrahim HAMID / AFP.

Mwezi Julai, ujumbe wa jeshi ulirudi nyumbani kwa mashauriano na kusema utaanza tena mazungumzo huko Jeddah yenye lengo la kurejesha amani nchini Sudan "baada ya kushinda vikwazo ." Marekani na Saudi Arabia, ambao walifadhili mazungumzo hayo, waliyasitisha muda mfupi baadaye.

Vita kati ya vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, vimeua zaidi ya watu 9,000 na kusababisha watu zaidi ya milioni 5.6 kuyakimbia makazi yao tangu vilipozuka mwezi wa Aprili.

Katika taarifa yake, jeshi limesema limekubali mwaliko kutoka Saudi Arabia na Marekani kwenda katika mji wa Jeddah huko Saudi Arabia "Jeshi linaamini kuwa mazungumzo hayo ni mojawapo ya njia zinazoweza kuumaliza mzozo huo".

"Kurejeshwa kwa mazungumzo haimaanishi kusitishwa kwa vita vya hadhi ya taifa, na kusitisha mapigano dhidi ya wanamgambo waasi," taarifa hiyo iliongeza.

Baadhi ya taarifa hii inatoka shirika la habari la Reuters na AFP

Forum

XS
SM
MD
LG