Duru za siasa na vyombo vya habari nchini Kenya vinasema huenda Kamisheni ya Tume Huru ya Uchaguzi wa Mipaka IEBC ikatangaza matokeo hayo Jumatatu.
Matokeo hayo yataamua iwapo rais aliyepo madarakani Uhuru Kenyatta ndiye mshindi wa upigaji kura uliofanyika Alhamis wiki iliyopita.
Kenyatta hakukabiliana na upinzani wowote katika uchaguzi huo wa marudio kufuatia kutenguliwa kwa matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti nane.
Iwapo tume hiyo itatangaza matokeo hii leo bado itakuwa na wajibu wa kuelezea idadi ya wapiga kura ambao walithibitishwa kupiga kura wiki iliyopita.
Katika zoezi hilo la kupiga kura vyombo vya habari viliripoti kuwa wafuasi wa upinzani waliwazuia wapiga kura kwenda kwenye vituo vya kupigia kura.