Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 12:59

Wakenya milioni 7.5 walipiga kura Alhamisi - IEBC


Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya, IEBC, ilitangaza Jumapili jioni kwamba Wakenya 7.4 walipiga kura kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika siku ya Alhamisi.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati, alisema kuwa kufikia saa moja jioni siku ya Jumapili, tume hiyo ilikuwa imepokea fomu 259 kati ya fomu 290 za 34B, ambazo zinahitajika kusafirishwa hadi kwenye kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura ya urais, kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya, mjini Nairobi.

Aidha Chebukati alisema kuwa licha ya kunukuliwa kabla ya uchaguzi kuanza akisema kuwa hakuwa na uhakika kama zoezi hilo lingekuwa la haki na kweli, sasa ana uhakika kuwa uchaguzi uliofanyika Alhamisi ulikuwa wa haki na ukweli.

Chebukati alisema maafisa wa tume hiyo walikuwa wanaendelea kuhakiki na kuthibitisha uhalisi wa fomu hizo kabla ya kutangaza matokeo ya urais.

Rais Kenyatta alikuwa anaongoza kwa Zaidi ya kura milioni 7.2. Uchaguzi huo wa urais, ambao umezua utata, ulifanyika siku ya Alhamisi licha ya mgombea wa upinzani, Raila Odinga, kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, kwa madai kwamba haungekuwa wa haki na wa kweli.

Tume ya IEBC inahitajika kikatiba kutangaza mshindi wa uchaguzi huo katika kipindi cha siku 7 tangu zoezi hilo lilipofanyika.

Wakati huo huo kiongozi wa upinzani Raila Odinga, siku ya Jumapili aliwashutumu wale wanaosema kuwa ni mzee mno kuendelea na siasa, na kusema kwamba hana nia ya kustaafu kutoka kwa siasa katika siku za karibuni.

"Mimi nitastaafu wakati niatataka na sihitaji kuambiwa na mtu nistaafu," alisema Odinga.

Odinga, mwenye umri wa miaka 72, ameahidi kutoa mwelekeo mpya kwa wafuasi wake siku kesho Jumatatu.

XS
SM
MD
LG