Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 00:00

Marekani yaanza usambazaji wa chanjo ya COVID-19


Marekani, Michigan, Portage, maboksi ya chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer na BioNTech yakiandaliwa kusambazwa nchini Marekani.
Marekani, Michigan, Portage, maboksi ya chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer na BioNTech yakiandaliwa kusambazwa nchini Marekani.

Shehena ya chanjo za virusi vya corona zilizoidhinishwa kutumika zinazohifadhiwa katika ubaridi wa hali ya juu zimeondoka kutoka katika kiwanda cha kampuni ya Pfizer huko Kalamazoo, Michigan, katika magari makubwa Jumapili kwa ajili ya kusafirishwa kwa ndege kwa haraka ili kufikishwa katika vituo mbalimbali nchini Marekani.

Chanjo hizo zinaweza kuanza kutolewa mapema Jumatatu wakati kuna ongezeko la maambukizi ya COVID-19 na Marekani inakaribia kufikia idadi ya vifo 300,000 kutokana na virusi hivyo, kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Virusi vya Corona cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Afisa mwandamizi wa operesheni inayojulikana kama Operation Warp Speed, program ya kutengeneza chanjo inayosimamiwa na utawala wa Trump, Jenerali wa Jeshi Gustave Perna, amesema katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi kuwa makampuni yatasafirisha chanjo za awali katika vituo vya usambazaji takriban 150, na vingine zaidi 450 au vituo kama hivyo vitapatiwa chanjo hiyo ifikapo Jumatano.

Idara ya Marekani ya Usimamizi wa Chakula na Dawa Ijumaa jioni iliidhinisha chanjo hiyo, iliyotengenezwa na kampuni ya kutengeneza dawa ya Marekani Pfizer na mshirika wake wa Ujerumani BioNTech, kwa ajili ya matumizi ya dharura. Chanjo hiyo, ambayo lazima ihifadhiwe katika ubaridi wa digrii -70 Celsius, imeonyesha kuwa ni inafanya kazi kwa asilimia 95 katika kuzuia COVID-19 katika majaribio ya hivi karibuni.

Wafanyakazi wa afya na wazee ambao wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu katika vituo vya kuwahudumia watakuwa wa kwanza kupatiwa dozi za kwanza milioni 2.9. Dozi mbili kila mtu, zitakazo tolewa kwa kupishana kwa muda wa wiki tatu kati ya dozi ya kwanza na ya pili, zinahitajika kwa kuzuia virusi vya COVID-19.

Afisa Mtendaji wa BioNTech Ugur Sahin amesema chanjo hiyo “itasaidia kuokoa maisha ya watu kote Marekani na inaweza kurejesha hali ya kawaida nchini.

Serikali Kuu ya Marekani inapanga kuongeza usambazaji wa chanjo katika wiki zijazo, hususan iwapo chanjo inayotengenezwa na kampuni ya Moderna Inc. Itaidhinishwa haraka.

Kikundi cha ushauri cha Kituo cha kudhibiti na Kuzuia Maradhi cha Marekani kilikutana Jumamosi na kupendekeza kuwa chanjo itumike kwa watu wenye umri wa miaka 16 na zaidi. Itatoa maelezo baadae iwapo makundi ya wanawake wajawazito na wale walio na umri wa chini ya miaka 16 wapatiwe chanjo hiyo.

Makundi hayo mawili hayakujumuishwa katika majaribio ya awali mpaka pale watafiti watakapoweza kufahamu iwapo chanjo hiyo ni salama kwa kiasi fulani kwa watu wazima wenye afya kabla ya kutumika kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Mtaalam wa ngazi ya juu wa magonjwa ya kuambukiza, Dkt Anthony Fauci, alisema Alhamisi kuwa wasimamizi na watengeneza dawa wataanza majaribio ya chanjo hizi Januari, kuangalia usalama wa chanjo kwa wajawazito na watoto.

Chanjo hii mara ya kwanza iliidhinishwa na Uingereza kutumika mapema mwezi huu, na wakazi wa Uingereza wakaanza kupokea chanjo hiyo Jumanne. Canada imeidhinisha pia matumizi ya chanjo hiyo na inatarajiwa kuanza kutolewa katika siku zijazo.

Bahrain, Mexico na Saudi Arabia pai wameidhinisha matumizi ya chanjo ya Pfizer.

XS
SM
MD
LG