Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:49

Saudi Arabia yataka G-20 kuhakikisha chanjo ya COVID-19 inasambazwa kwa usawa


Mkutano wa G-20 unaomalizika Jumapili kwa njia ya mtandao.
Mkutano wa G-20 unaomalizika Jumapili kwa njia ya mtandao.

Mkutano wa kikundi cha nchi 20 tajiri duniani unaendelea kwa njia ya mtandao leo Jumapili nchini Saudi Arabia. 

Rais wa Marekani Donald Trump ambaye hajaonekana mara nyingi hadharani tangu kushindwa uchaguzi wa rais mapema mwezi huu, amepangiwa kushiriki katika mkutano huo Jumapili, kama alivyohudhuria siku ya Jumamosi.

Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Mfalme wa Saudi Arabia Salman alifungua mkutano Jumamosi kwa kuwataka nchi wanachama kuuhakikishia ulimwengu upatikanaji wa chanjo ya gharama nafuu na kusambazwa kwa usawa.

“Hatutasita kufanya juhudi kuhakikisha chanjo ni ya gharama nafuu na inapatikana kwa watu wote, sambamba na ahadi ya nchi wanachama kutoa motisha ya ubunifu,” viongozi hao walisema katika rasimu ya makubaliano ya waraka wa pamoja wa G-20 ambao Shirika la habari la Reuters umeuona. “Tunatambua jukumu la chanjo itakayo wafikia wengi zaidi kama ni kitendo kizuri kwa umma duniani.”

Janga la COVID-19 na kudorora kwa uchumi vilitawalia siku ya kwanza ya mkutano huo wa siku mbili kwa njia ya mtandao wa nchi 20 tajiri zaidi na nchi zenye kuinukia kiuchumi.

“Tunajukumu kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja wakati huu wa mkutano huu na kutoa ujumbe mzito wa matumaini na uhakikisho,” Salman amesema akifungua mkutano huo.

Maelezo hayo ya mfalme yamejiri wakati maambukizi ya virusi vya corona yamefikia milioni 58 milioni na vifo vinavyotokana na janga hilo vimekaribia milioni 1.4, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Viongozi wa G-20 wana wasiwasi kuwa janga hili litaongeza mwanya kati ya nchi tajiri na maskini.

Ili kukabiliana na hali hii, Umoja wa Ulaya umesihi michango ya jumla ya dola za Marekani bilioni 4.5 kuwezesha mradi wa kimataifa kuharakisha utengenezaji na usambazaji wa chanjo, vipimo na tiba, kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi takriban dola milioni 593. Rais Vladimir Putin wa Russia amejitolea kuchangia chanjo aina ya Sputnik V dhidi ya COVID-19 na China imeahidi kushirikiana katika utengenezaji wa chanjo.

Chansela Angela Merkel
Chansela Angela Merkel

Siku ya Jumamosi, Trump aliandika katika Twitter juu ya wizi wa kura usiokuwa na ushahidi wa uchaguzi wa Marekani wa Novemba 3 wakati Salman akizungumza kabla ya kuondoka kuelekea kucheza golf katika klabu yake kaskazini mwa Virginia.

Msemaji wa White House Kayleigh McEnany amesema Trump alizungumzia haja ya kushirikiana kurejesha ukuaji wa uchumi, lakini msemaji huyo hakutaja ahadi ya Marekani kusaidia usambazaji wa chanjo hiyo ulimwenguni katika muhtasari uliotolewa jioni Jumamosi.

Baada ya Trump kuondoka katika mkutano huo wa mtandaoni, Waziri wa Fedha wa Marekani Steve Mnuchin, ambaye alihudhuria mkutano, amesema katika tamko la hazina kuwa Juhudi za Kusitishwa kwa Malipo ya Madeni kwa miezi saba “ ni mafanikio muhimu ya G-20 ikiwa ni majibu kwa janga hilo.”

Waziri Steve Mnuchin
Waziri Steve Mnuchin

Hatua hiyo inalenga kuzisaidia nchi maskini sana duniani kukabiliana na athari za janga hilo hadi katikati ya mwaka 2021.

Taarifa ya Wizara ya Fedha pia imesema Muundo huu wa Pamoja wa G-20 utazisaidia nchi maskini sana kutatua matatizo ya deni yanayotokana na janga hilo “kwa kuratibu ufumbuzi wa deni la kila nchi ikiwa itahitajika.”

Mkutano huo kwa kiasi kikubwa unafanyika mtandaoni kwa mara ya kwanza kwa sababu ya janga la COVID-19

Nchi wanachama wa G-20 ni pamoja na Argentina, Australia, Brazil, Uingereza, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italy, Japan, Mexico, Russia, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Nchi hizi zinawakilisha, kwa mujibu wa tovuti ya kikundi hiki cha G-20 “takriban asilimia 80 ya uzalishaji wa uchumi duniani, theluthi mbili ya wakazi wa duniani na robo tatu ya biashara za kimataifa.”

XS
SM
MD
LG