Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 03:35

Tanzania yaomboleza vifo vya wahanga 35


Maombolezo Arusha
Maombolezo Arusha

Miili 35 ya wahanga wa ajali ya barabarani imeagwa kitaifa leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid wakati madereva wakikumbushwa kuhakikisha wanabeba watu kulingana na uwezo wa gari na kuwa makini wanapokuwa wapo barabarani.

Huzuni na simanzi

Wakati maombolezo yanaendelea vilio vilitawala hapo uwanjani hali ya kwamba baadhi ya wafiwa walianguka na kupoteza fahamu.

Viongozi wa dini zote walishiriki katika zoezi hilo la kuendesha ibada ya maombolezo hayo kuombea roho za marehemu waliotangulia mbele ya haki.

Uwanja ulikuwa na ulinzi mzito wakati wa maombolezo hayo ambapo askari wa kutuliza ghasia walikuwa wamesambazwa sehemu zote za uwanja.

"Pigo hili kubwa linatukumbusha kufanya marekebisho mengi...na kutokana na kasoro hizo zinaleta maafa kama haya," amesema Makamu wa Rais huko Arusha.

“Naomba kupaza sauti yangu kwa ndugu zangu madereva kuwa waadilifu na kuwa makini wanapokuwa barabarani ,” ameeleza Samia Suluhu wakati akiwakilisha salamu za Rais John Magufuli kwa umma wa Watanzania Jumatatu.

Suluhu ameahidi kuwa atahudhuria maziko ya wale ambao ni wakazi wa Arusha na ambao miili yao itazikwa hapa mkoani.

Watalii wapongezwa

Makamu wa Rais amewashukuru sana watalii waliokuwa wakipita eneo la ajali na kutoa msaada wao mara mmoja.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa watalii hao ni madaktari na wamekuwa wakishirikiana na madaktari wetu hadi sasa kuwatibu majeruhi 3 waliopo hospitali na wameahidi kuwapeleka hadi nje ya nchi kwa matibabu pale itakapobidi.

Kenya yamtuma mwakilishi

Katika maombolezo hayo serikali ya Kenya imemtuma Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Dr Fred Matiang’i kuja kuiwakilisha katika maombolezi na kuiaga miili ya wanafunzi, walimu na dereva wao ambao walipoteza maisha katika ajali ya Jumamosi.

Katika ajali hiyo wanafunzi wa darasa la saba, walimu na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vincent ya Arusha wote walipoteza maisha baada ya basi waliokuwa wakisafiria kutumbukia katika korongo.

Basi hilo lilikuwa limebeba waalimu 3 na dereva, msaidizi wake na wanafunzi 27. Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la shule kutumbukia katika korongo refu la mto Marera wilayani Karatu.

Viongozi wahudhuria mazishi

Vyanzo vya habari mkoani Arusha vimeripoti kuwa mamia ya watu wamehudhuria na kutoa salamu za rambirambi wakiwemo mkuu wa mkoa wa Manyara, Joel Bendera, kaimu jaji mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamisi Juma, Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene na Waziri wa Fedha, Philip Mpango.

Wengine zaidi ni pamoja na katibu mkuu wa CCM Abdurahamani Kinana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe.

Misaada mbali mbali tayari imefika na gaharma zote za usafiri, majeneza 35 pamoja sanda zimelipwa na mkoa.

Wabunge wachangia msiba

Aidha wabunge wamekubali kukatwa posho za siku mbili kwa ajili ya kutoa rambirambi kwa wazazi wa watoto hao. Kwa siku mbunge analipwa Sh 220,000 kama posho ya kikao.

Kwa mujibu wa taarifa za Mkoa, Kampuni ya Ngorongoro wametoa 15m/-, Tanapa 20m/-, Auwasa 1m/-, AICC 5m/- na jiji la Arusha 5m/-.

Miili ya watu 35 ililetwa na gari la jeshi la Wananchi na utaratibu wa kuaga maiti hizo ulifanyika kwa heshima zote za kitaifa.

Pia kulikuwa na wawakilishi wa Walimu 30 toka serikali ya mapinduzi Zanzibar katika maombolezo hayo.

Aidha vikosi vyote vya usalama likiwemo jeshi la Magereza, jeshi la wananchi na Polisi walishiriki katika maombolezo hayo.

XS
SM
MD
LG