Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 00:25

Wamiliki wa malori Tanzania wakerwa na urasimu


Rais Magufuli alipotembelea bandari ya Dar es Salaam
Rais Magufuli alipotembelea bandari ya Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa), Angelina Ngalula amelalamikia juu urasimu uliopo bandari ya Dar es Salaam ambao unafanya mzigo kukaa bandarini siku kumi hadi 13 huku nchi nyingine wakitumia siku tatu hadi nne.

“Vitu ambavyo vinatukwamisha ni pamoja na tunapoteza muda mwingi bandarini jambo ambalo linatufanya tukose ushindani, naipongeza TPA wameboresha huduma kwa sasa wanafanya kazi masaa 24 wengine hawafanyi wanatukwamisha,” alisema Angelina.

Alisema tatizo lililopo bandarini hakuna mratibu kuna taasisi nyingi ambazo pia zina mifumo yao huku wengine wafanyabiashara inabidi kuwafata katika ofisi zao ambazo hazipo bandarini.

Wakati huo huo Rais John Magufuli ameagiza kuanzia kesho taasisi zote zinazotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam ziungane na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kutoa huduma kwa saa 24 ili kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuongoza Mkutano wa 10 wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, Dar es Salaam. “Kama alivyosema Waziri Mkuu, tunataka kufanyia kazi maoni yenu mara moja, kuanzia Jumatatu nataka taasisi zote za pale bandarini zitoe huduma saa 24, haiwezekani bandarini kwetu mizigo ichukue siku 13 kuitoa wakati bandari za wenzetu majirani inatoka baada ya siku tatu, tutashindana vipi?”

Rais alikuwa akijibu maoni ya wafanyabiashara hao ikiwemo tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini na hivyo kuagiza kuanzia kesho taasisi zote katika bandari ya Dar es Salaam na TPA kufanya kazi kwa saa 24.

Akijibu hoja ya Tatoa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikiri kuwepo na urasimu mkubwa bandarini ambapo sekta ambazo zinafanya kazi zinakwamisha wafanyabiashara katika kutoa mizigo yao.

“Kuna urasimu wa hovyo sana bandarini, sekta ambazo hazifanyi kazi hatukubaliani nazo, kama TPA wanafanya kazi saa 24 kwanini TRA, TFDA, TBS, ningependa kupata taarifa Jumatatu kwamba hao wengine wanakesha sambamba na TPA,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Tanzania imelalamikiwa utendaji kazi wake katika bandari uko chini, alisema kama TPA wanafanya kazi saa 24 lakini mzigo utakwama kwa sababu taasisi hizo nyingine zinafanya kazi saa chache.

Alisema bandari ya Mombasa mzigo unachukua siku saba hadi nane kutoka bandarini wakati Bandari ya Dar es Salaam ni siku 13 ambapo alimtaka Waziri wa fedha ahakikishe TRA inafanya kazi saa 24.

Aliahidi wawakilishi wa sekta binafsi waliohudhuria mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha maoni yao yote yanafanyiwa kazi ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali zake na kusonga mbele kimaendeleo.

“Naomba niwahakikishie kuwa hisia zenu tumezipata, maoni yenu tutayazingatia na tutahakikisha tunayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kwa pamoja tufanye kazi ya kuijenga nchi yetu,” alisema Majaliwa.

XS
SM
MD
LG