Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:40

Makanali wawili wa jeshi wawekwa kizuizini Madagascar


Rais wa Madagaska Andry Rajoelina (wa pili kulia) akipiga kura katika kituo cha Ambatobe, Antananarivo, Novemba 16, 2023, Picha na MAMYRAEL / AFP
Rais wa Madagaska Andry Rajoelina (wa pili kulia) akipiga kura katika kituo cha Ambatobe, Antananarivo, Novemba 16, 2023, Picha na MAMYRAEL / AFP

Makanali wawili wa jeshi la Madagascar wamewekwa kizuizini na kushtakiwa kwa kuchochea uasi wakati wa uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo, mwendesha mashitaka mkuu na wapelelezi walisema siku ya Jumanne.

Mashtaka hayo yalitangazwa siku tatu tu baada ya Andry Rajoelina kushinda muhula mpya wa rais wa kisiwa hicho cha Afrika katika uchaguzi ambao ulisusiwa na viongozi wengi wa upinzani.

Watuhumiwa hao wawili walifunguliwa mashitaka rasmi siku ya Jumatatu kwa "kutishia usalama wa serikali", alisema mwendesha mashitaka wa Antananarivo Narindra Rakotoniaina.

Wamewekwa ndani hadi kesi itakaposikizwa Januari 16.

"Makanali wawili wa jeshi walijaribu kuwaunganisha makamanda wa kikosi katika mji wa Antananarivo kwa lengo la kuwachochea kufanya uasi," Tahina Ravelomanana, mkuu wa kitengo cha uhalifu Madagascar, aliliambia shirika la habari la AFP.

Walichukua hatua "kuleta ushindani katika uchaguzi na kuvuruga mamlaka".

Kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi mnamo Novemba 16, maafisa hao wawili walitoa kiasi cha dola 27,500 kwa viongozi kadhaa wa jeshi ili wawachochee wanajeshi kuleta matatizo, Rakotoniaina alisema.

Viongozi hao wa jeshi walikataa hongo hiyo na wakaripoti makanali hao wawili kwa wakuu wa majeshi, ambao waliamuru uchunguzi ufanyike, aliongeza.

Rajoelina alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi, bila duru ya pili kuhitajika.

Ni mara chache uchaguzi za Madagaska kumalizika bila malumbano. Rajoelina alikua rais kwa mara ya kwanza mwaka 2009 wakati Marc Ravalomanana alipolazimishwa kuondoka madarakani. Alishinda uchaguzi wa kwanza mwaka 2018.

Chanzo cha habari ni Shirika la habari la AFP

Forum

XS
SM
MD
LG