Maandamano haya yanayo fanywa na wanawake yalianza kufanyika mwaka 2017, siku moja baada ya Donald Trump kuapishwa kuwa rais wa Marekani.
Siku ya kwanza kamili ya utawala wa Rais Trump, mamia ya maelfu ya wanawake waliteremka jijini Washington kuonyesha upinzani wao mkubwa dhidi ya utawala mpya na sera zake.
Maandamano kama hayo pia yalifanyika katika maeneo zaidi ya 600 ndani ya Marekani na duniani kote kuunga mkono maandamano yaliyokuwa yanafanyika mjini Washington.
Peter Newsham, kaimu mkuu wa polisi Washington kwa wakati huo, alisema kuwa maandamano hayo katika mji mkuu wa Marekani, “ni msongamano mkubwa hadi hivi sasa na hakuna hata nafasi tena ya kuandamana.”
Wengi wa wanawake hao walikuwa wamevaa kofia zilizofumwa katika umbile la “paka”, ikiwa na masikio madogo yap aka, kuonyesha kuunga mkono hisia zilizoko dhidi ya Trump na kukosoa maoni ya Trump yenye lugha chafu aliyokuwa ameyatoa miaka kadhaa huko nyuma kabla ya kuingia katika medani ya siasa.