Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:12

Maafisa 5 wa NEMC wafunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi


Maafisa watano wa NEMC wafikishwa mahakamani.
Maafisa watano wa NEMC wafikishwa mahakamani.

Maafisa watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), wamefikishwa Alhamisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Tanzania, wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ya uhujumu uchumi.

Maofisa hao waliofikishwa kortini Jumatano ni Deusdedith Katwale (38), Lilian Laizer (27), Luciana Lawi (33), Edna Lutanjuka (51) na Mwaruka Miraji (42). Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mbando.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote.

Mashtaka mengine yanayowakabili ni kula njama kutenda kosa la kughushi, kuwasilisha hati bandia na kusababisha hasara kwenye mamlaka husika.

Hakimu huyo aliwaambia washtakiwa kuwa, mashtaka yanayo wakabili yanaangukia katika sheria ya uhujumu uchumi, hivyo haina mamlaka ya kuisikiliza, mpaka itakavyoamuriwa vinginevyo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kufuatia hali hiyo, hakimu aliwaamuru kubaki mahabusu hadi Novemba 14, mwaka 2018 kesi hiyo itakapotajwa kwa kuwa upelelezi, kwa mujibu wa upande wa mashtaka, haujakamilika.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Faraja Ngoka, alidai kati ya Septemba 27, 2016 na Aprili 6, 2018, jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikula njama kutenda kosa la kughushi.

Alidai kuwa Oktoba 17, 2017, maofisa wa NEMC kwa nia ya kudanganya walighushi cheti cha tathmini ya mazingira wakidai kuwa kilikuwa halisi wakati si kweli.

Mahakama ilielezwa na upande wa mashtaka kuwa, katika kipindi hicho hicho jijini Dar es Salaam, maofisa hao walighushi saini ya Makamba kwenye cheti hicho wakidai kuwa ilikuwa ni saini yake, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Ilidaiwa zaidi kuwa, Oktoba 2017, makao makuu ya NEMC jijini Dar es Salaam, Edna anadaiwa kuwasilisha cheti hicho kwa Deogratius Chacha, akidai kuwa, kimetolewa na NEMC, wakati si kweli.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kati ya Septemba 27, 2016 na Aprili 6, 2018, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote walijipatia Sh. milioni 160 kutoka kampuni ya PMM Estate (2001) LTD, kwa kudanganya kuwa wangefanya tathmini ya mazingira na kumpatia cheti kinachohusika wakati si kweli.

Inadaiwa pia, katika kipindi hicho hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote waliisababishia hasara NEMC jumla ya Sh. milioni 160.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka uliomba kutoa hati ya kumkamata ofisa mwingine wa NEMC, Magori Wambura, ambaye anakabiliwa na mashtaka kama hayo. Mahakama iliridhia maombi hayo na kuamuru akamatwe.

XS
SM
MD
LG