Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amefurahishwa na kupelekwa tena kwa wanajeshi wa Marekani nchini kwake ambako mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa al-Shabaab yanaongezeka wakati wa mzozo wa uchaguzi uliocheleweshwa.
Jumatatu, utawala wa Rais Joe Biden ulitangaza mipango ya kutuma wanajeshi 600 wa Marekani kusaidia operesheni zinazowalenga wanamgambo wa Kiislamu wenye msimamo mkali wa al-Shabaab.
Rais huyo mpya ameiambia VOA kwamba kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kurejesha usalama na kumaliza mapigano ya ndani ambayo yamedhoofisha taasisi za Somalia.
Rais wa Somalia ameeleza:“ Hiyo ilikuwa ni hatua ya muhimu iliyochukuliwa katika mwelekeo bora na rais wa marekani Biden. Marekani ni nchi kubwa inayounga mkono na mfadhili mkubwa wa somalia katika masuala ya kibinadamu na zaidi ya hapo Marekani ni mfadhili mkubwa katika usalama na ulinzi , kwa kufanya hivyo na kubadilisha uamuzi wa awali wa rais wa zamani Donald Trump umekuwa ni uamuzi wa muda muafaka na mzuri sana.
Watu wa somalia wanapokea hilo vizuri sana, na tunatazamia kupokea msaada huo. Marekani siyo tu inatuma pesa na vifaa lakini wanatupa damu yao na maisha yao kuwakomboa wengine.”
Kuhusu suala la ukame, Rais huyo mpya amesema atateua mjumbe maalumu.
Rais Mohamud ameeleza kuwa: “Ndio ukame ni mgumu sana. Nitamteua mwakilishi maalum kwa ajili ya ukame nchini na pia huu ni wakati mgumu sasa, watu wamepoteza mifugo yao, siyo tena aina ya zamani ya kilimo na uzalishaji.
Kwa hiyo Somalia haiko katika hatari ya usalama wa al-Shabaab na usalama wa kimwili tu lakini pia usalama wa chakula. Hilo ni suala zito la usalama na litakuwa sehemu ya usalama wa jumla wa Somalia. Kwa hiyo Marekani ndiye mfadhili mkubwa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya Somalia.”