Waendesha mashtaka katika kesi ya mtanzania Ahmed Ghailani wamemueleza kua ni muuwaji wa halaiki ya watu katika mashambulio mawili ya mabomu ya 1998 dhidi ya ubalozi wa Marekani huko Nairobi na Dar es Salaam. Waendesha mashtaka walitoa maelezo hayo jana katika mahakama ya serikali kuu ya Marekani mjini New York walipokua wanatoa hoja za kukamilisha mashtaka yao.
Naibu mwendesha mashtaka wa Marekani Harry Chernoff alipinga dai la watetezi kwamba Ahmed Ghailani alirubuniwa na wanachama wa al Qaida katika mpango wao wa kushambulia kwa mabomu ubalozi wa Marekani huko Kenya na Tanzania.
Chernoff alirudia kueleza ushahidi na matamshi ya mashahidi ambayo yanaonesha Ghailani alihusika katika njia mbali mbali za mango huo. Anasema ghailani alitambuliwa kuwepo katika maeneo mjini Mombasa na Dar es salaam na wenzake katika njama hiyo.
Mwendesha mashtaka alikumbusha ushahidi ulotolewa na wataalamu wa FBI, walogundua mabaki ya miripuko katika maeneo hayo pamoja na hati zinazo onesha kwamba mtetezi alikuwepo huko. Mtaalam wa FBI alieleza kwamba aligundua funiko la kuripua ndani ya kabati aliyotumia Ghailani.
Chernoff vile vile alitaja ushahidi wa majirani walokumbusha kwamba duka moja la nguo la Mombasa lililokua wakati mmoja biashara inayonawira, liligeuka na kua maficho ya siri ambako Ghailani na washirika wake wa kigeni walotambuliwa kua ni washirika walopanga njama hiyo.
Mwendesha mashtaka alisisitiza juu ya ushahidi wa mfanya biashara aliyemtambua Ghailani kama mtu aliyejaribu kujadili juu ya bei ya lori iliyotumiwa katika shambulio la Dar es Salaam.
Mwendesha mashtaka Chernoff, alikumbusha alama ya kidole cha Ghailani iliyopatikana kwenye bill ya simu ya mkono iliyokua imeandikishwa kwa jina lake. Simu hiyo ilitumiwa mara ya mwisho kiasi ya masaa mawili kabla ya shambulio na mjitoa mhanga aliyeendesha lori hadi ubalozini.
Baraza la mahakimu lilikumbushwa pia juu ya paspoti ya bandia iliyokua na picha ya Ghailani na tiketi zilizokua na jina hilo la bandia ambayo alitumia kusafiria hadi Pakistan siku moja kabla ya mripuko. Ushahidi zaidi umeonesha maafisa waandamizi wa al-Qaida walikua ndani ya ndege aliyosafiria Ghailani.
Wakili wa Ghailani hakumita shahidi hata mmoja. Na mtetezi mwenyewe alikata pia pendekezo la Jaji Lewis Kaplan kwamba atoe ushihidi kujitetea mwenyewe. Upande wa watetezi wanatazamiwa kutoa hoja zao za mwisho siku ya Jumanne.